Thursday, 18 September 2014

Wanafunzi wadungwa sindano kuzuia mimba


NA MWANDISHI WETU
WAKATI taifa likihaha kusaka tiba ya mimba za utotoni ili kuwezesha watoto wa kike kupata elimu, baadhi ya wauguzi wilayani Newala, Mtwara, wameibuka na mbinu mpya.
Wauguzi hao wanadaiwa kuwachoma sindano za uzazi wa mpango wanafunzi wa shule za msingi, kinyume cha utaratibu kwa lengo la kuwakinga na mimba zisizotarajiwa.
Hayo yamebainika kupitia taarifa ya Matokeo ya Ripoti ya Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA). 
TAMWA iliendesha utafiti maalumu kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia katika wilaya 10 nchini, kuanzia mwezi Mei, mwaka huu. 
Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa baadhi wasichana walishindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya ujauzito, jambo ambalo kwa sasa wenyeji wa Newala wamesema limekuwa historia.
Hatua hiyo inatokana na matumizi ya sindano za uzazi wa mpango,  mkakati ambao umekuwa ukiendeshwa kwenye baadhi ya shule wilayani humo.
“Baada ya kuona wasichana wengi wanaishia darasa la tano kwa kupata ujauzito, sasa wanachomwa sindano za uzazi wa mpango na huo ni ushauri wa wazazi ama wanaume wenye mahusiano nao,” alisema mkazi mmoja wa kijiji cha Luchungu wilayani Newala.
Ofisa mmoja wa afya (jina linahifadhiwa) wa Zahanati ya Makote, wilayani humo, alithibitisha jambo hilo na kusema kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto kupatiwa huduma kuwezesha kuhitimu elimu ya msingi.
Akizindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa TAMWA, Rose Reuben, alisema ripoti imebainisha kupungua kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia nchini, ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na  mwamko wa wanawake.
Alisema wanawake wengi wamekuwa wakipatiwa elimu ya masuala kupitia vyombo vya habari nchini, hivyo kupungua kwa matukio hayo.
“Kabla ya kuanza utafiti huu mwaka 2011, takwimu za idadi ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyoripotiwa, hazikuwa sahihi kama ambavyo matokeo ya utafiti yanavyoonyesha,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi wa TAMWA, Gladness Munuo, alisema takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi nchini, isipokuwa wilayani Ilala, Dar es Salaam, ambapo mwaka jana yalikuwa 124 na mwaka huu yameongezeka hadi 310.
“Katika wilaya ya Ilala, matukio ya kubakwa ndio yameonyesha kushika kasi zaidi kuliko aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa watoto watano hulawitiwa kila siku,” alisema.
Akizungumzia madhara ya dawa za uzazi wa mpango, Dk. Magreth Mathew wa Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, alisema watu wengi wanapotumia, hujiona wapo huru na salama, hivyo kuruhusu wengine kufanya ngono zembe.
Alisema dawa hizo zinapoingia kwenye mwili wa binadamu, mpangilio wa homoni huvurugika hadi muda wake unapokwisha, ndipo mwili hurejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Dawa hizo zina madhara yake, kwani wengine hawawezi kupata ujauzito katika hali ya kawaida hadi wapatiwe matibabu. Hii inatokana na miili kutofautiana homoni, ingawa kwa wengine hurejea baada ya dawa kwisha nguvu,” alisema.
Madhara mengine ni mtumiaji kuumwa kichwa, tumbo, kupata hedhi kwa wingi bila mpangilio maalum ama wakati mwingine kutopata hedhi kabisa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru