Wednesday, 10 September 2014

Serikali ya kijiji Ruvu yadaiwa kuuza shamba kinyemela


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WANANCHI wa kitongoji cha Ruvu darajani, wilayani Bagamoyo, wameilalamikia serikali ya muda ya kitongoji cha Ruvu, kata ya Vigwaza,  kwa kuuza shamba la ekari 10 mali ya kijiji.
Imeelezwa kuwa shamba hilo limeuzwa kwa maslahi binafsi na bila kuwashirikisha wana kijiji.
Mwana kijiji, Athumani Mkali, alisema  uongozi wa muda wa kijiji cha Ruvu kuuza eneo hilo ni batili. “ Ukizingatia pia baadhi ya wananchi wengi hawana maeneo ya makazi na mashamba, leo eneo linauzwa kwa mtu mwingine, si haki,” alisema.
Alisema eneo hilo la ekari 10, limetolewa kwa mwekezaji huyo kinyemela na inasemekana limeuzwa kwa sh. milioni 50, ambapo mwekezaji huyo ametoa ahadi ya kuwajengea vyumba vya zahanati yenye thamani ya sh.milioni 25, jambo ambalo wananchi hawakubaliani nalo.
Naye Hemed Idd, alisema kuuzwa kwa  eneo la kijiji kwa faida binafs ni ukiukwaji wa sheria za serikali za mitaa.
Alisema jambo hilo likifumbiwa macho linaweza kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi kunakofanywa na uongozi huo .
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, alipoulizwa suala hilo alisema  hajui uwepo wa mgogoro huo, ila atawasiliana na katibu tarafa wa eneo hilo kujua kinachoendelea.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru