Thursday 11 September 2014

Yona ajitetea, amtaja Mkapa


Na mwandishi wetu
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ameileza mahakama kuwa mchakato wa kumpata mkaguzi wa madini ya dhahabu ulifuata utaratibu zote na kusimamiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Yona ambaye jana alipanda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuanza kujitetea, alidai mwaka 2002 kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu mapato ya dhahabu iliyokuwa ikichimbwa na kampuni tano za kigeni.
Akiongozwa na wakili wake Elisa Msuya mbele ya Jopo linaloongozwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Msajili Saul Kinemela, alidai wizara iliamua kuhakiki gharama za madini hayo kwa kuwa BoT ndiyo iliyokuwa ikisimamia akaunti za kampuni hizo.
Alidai kuwa ilikubaliwa kutafutwa kwa mkaguzi wa dhahabu, ambapo mchakato huo ulisimamiwa na BoT na Wizara ya Nishati na Madini.
Aliendelea kudai baada ya majadiliano aliamua kumuandikia Rais aliyekuwepo wakati huo, Benjamin Mkapa dokezo kuhusu ukaguzi wa dhahabu Mei 11, 2003.
Alidai alimfahamisha Rais Mkapa majadiliano waliyofanya kati ya Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, BoT na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanaendelea vizuri.
Yona alidai Machi 3, mwaka 2003 alimuandikia Rais dokezo kwa mara ya kwanza kumfahamisha kwa maandishi, akiomba aruhusu kutekeleza ukaguzi wa dhahabu kwa kufuata taratibu na sheria.
Alidai Machi 20, 2003 Rais aliandika majibu kwamba anakubali waendelee na mchakato haraka.
“Tulimuahidi Rais kwamba mchakato utazingatia mapato ya nchi na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kweli katika hilo tulizingatia ushauri wa AG,” alidai.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo hakuweza kuendelea na ushahidi baada ya Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya kupinga kupokelewa kwa kielelezo kutoka ofisi ya AG.
Jopo hilo kwa pamoja lilikubaliana kuahirisha hadi leo kwa ajili ya kumpa nafasi Wakili Oswald kujiridhisha na kielelezo hicho.
 Washtakiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali harasa ya sh. bilioni 11.7.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo Agosti, 2002 kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart ya nchini Uingereza kinyume cha sheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru