Tuesday, 2 September 2014

Bendera awataka wanahabari kuunga mkono jitihada za TMA


NA WILLIAM SHECHAMBO
MKUU wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, amewataka wanahabari nchini kutumia nafasi waliyonayo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa manufaa ya taifa.
Amesema jitihada hizo, ambazo ni utoaji wa taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakati na uhakika, haziwezi kuwafikia walengwa bila kuwepo vyombo vya habari ambavyo huunganisha jamii, serikali na taasisi binafsi.
Bendera alitoa rai hiyo jana mkoani Morogoro, wakati akifungua warsha ya wanahabari iliyokuwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa usahihi kama inavyokusudiwa na TMA.
Alisema umefika wakati kwa wanahabari kufahamu zaidi juu ya umuhimu wao katika jamii, katika kuleta maendeleo ya taifa katika sekta mbalimbali, ambapo hali ya hewa ni suala mtambuka linalogusa kila nyanja inayoweza kuchangia maendeleo ya nchi kwa kiasi kikubwa.
Mkuu huyo wa mkoa alisema TMA wanafanya kazi nzuri ya kujulisha umma juu ya mabadiliko na maendeleo tofauti ya hali ya hewa nchini.
Alisema binafsi amekuwa akipata taarifa kutoka kwenye mamlaka hiyo, ambazo huzisambaza katika wilaya zote za mkoa wake kupitia wakuu wa wilaya ili kuwa macho na masuala ya hali ya hewa.
“TMA wanajitahidi, lakini hawawezi bila nyie wanahabari. Binafsi ninapata taarifa za kimaandishi kutoka TMA, ambazo huwa nazisambaza kwa wakuu wangu wa wilaya ili wajiandae na wachukue tahadhari za kimakusudi na hii imekuja baada ya mafuriko ya Dumila,” alisema Bendera.
Aliongeza kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kupuuzia taarifa za hali ya hewa, hivyo aliwasihi wanahabari kuwa kiungo cha kubadili mitazamo yao ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa maafa makubwa.
Aidha, aliwataka TMA kutumia lugha nyepesi kwenye taarifa zao kwa umma ili ziweze kueleweka na wanahabari kwa lengo la kusambaza ujumbe bila upotoshaji kama ilivyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema wanalifanyia kazi suala la kurahisisha lugha kutoka ile ya kitaalamu zaidi na kuwa nyepesi ili wanahabari waielewe na kuiwasilisha kwa jamii kama inavyokusudiwa.
Warsha hiyo inaambatana na utoaji wa utabiri wa msimu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu, unaofanyika kesho mkoani humu, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nje ya mkoa wa Dar es Salaamn

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru