Thursday, 18 September 2014

Mbowe aufyata  • Ajisalimisha Polisi kuhojiwa, Tundu Lissu amzuia
  • Wanavyuo wamvaa , Bunge kama kawaida 
  • Changoja acharuka, maandamano ni marufuku
  • LHRC yachoshwa, yakemea kauli za uchochezi

Na waandishi wetu
JESHI la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini, ikiwa ni pamoja na kuonya kuwa hakuna mtu atakayeingia barabarani kuandamana atayevumiliwa.

Habari za kuaminika zinasema kuwa, wafuasi na viongozi wa CHADEMA katika mikoa mbalimbali, wamejipanga kufanya maandamano leo, ikiwa ni maagizo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe ametii amri ya Jeshi la Polisi baada kutakiwa kufika Makao Makuu kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na kauli zake za uchochezi zinazolenga kuvuruga amani ya nchi.
Hata hivyo, Mbowe anajisalimisha polisi leo baada ya kutakiwa na Kamati Kuu ya CHADEMA kuitikia wito huo, baada ya awali Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, kumzuia kwa kuhofia nguvu ya dola kutokana na kauli alizotoa.
Jana, Lissu alikiri mbele ya waandishi wa habari kuwa, alimzuia Mbowe kujisalimisha polisi, wakati ambao tayari kiongozi huyo na chama chake wameshapokea barua ya wito kutoka jeshi hilo.
Mbowe atasindikizwa na baadhi ya viongozi na wanasheria wa CHADEMA, akiwemo, Lissu, Halima Mdee, Mabere Marando, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari.

Polisi yacharuka
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, alisema wana taarifa za uhakika kuwa CHADEMA wamepanga kufanya maandamano leo.
Alionya polisi hawatasita kuchukua hatua kali na kwa mujibu wa sheria kwa yeyote ambaye atajaribu kuvunja sheria.
Kamishna Chagonja, alitoa msimamo huo ikiwa ni mara ya pili jana, alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo alionya kuwa kauli za Mbowe haziwezi kuachwa zikapita kama upepo.
“Tumeanza kupokea maombi ya CHADEMA kikitaka kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kifupi ni kinyume cha sheria na hayaruhusiwi,” alisema Chagonja.
Alisema maandamano hayo ni batili kwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, lipo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hakuna sheria iliyokiukwa.
“Kitendo cha kufanya maandamano kushinikiza kuvunjwa kwa bunge hilo ni kinyume cha sheria, jambo ambalo hatutalivumilia hata kidogo,” alisema na kuongeza: “Jeshi la Polisi lina jukumu la kulinda watu wote.”
Pia alisema kuna kesi inayoendelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, inayohoji uhalali wa bunge hilo, ambayo haijafika mwisho na kutolewa uamuzi, hivyo maandamano hayo ya CHADEMA ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Haki za Binadamu wachoshwa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimewaonya wanasiasa kuacha mara moja kutoa kauli za kupotosha jamii na zenye kebehi kwa kuwa hazijengi.
Kimewataka kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi katika Bunge Maalumu la Katiba na kwamba, mchakato huo unavurugwa na wachache wasio na mapenzi mema kwa taifa.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio, aliyasema hayo mjini Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.  Hellen Kijo Bisimba.
“Tunawataka wanasiasa kuacha kutoa kauli za kupotosha jamii, kwa kuwa hazitajenga bali ni kuwavuruga wananchi,” alisema.
Pamoja na tamko hilo, Urio alisema bunge hilo linahitaji kura 16 kutoka Zanzibar ili kutimiza namba ya theluthi mbili ya wajumbe ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa.
Alisema kwa sasa akidi haiwezi kutimia kutokana na masharti ya kifungu namba 26 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambacho kinataja akidi kuwa ni theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema Rais Jakaya Kikwete kwa nafasi yake kikatiba, ana nguvu ya kuteua wajumbe wengine wa bunge hilo, hivyo ni vyema akatumia nafasi hiyo ili kutafuta mwelekeo mpya.

Wanachuo wamvaa Mbowe
WANAFUNZI wa Vyuo vya Elimu ya Juu, wamepinga na kulaani vikali kauli ya Mbowe kuhamasisha vurugu na migomo isiyo na tija nchini.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Dar es Salaam, Musa Omar, alisema jana kuwa, kauli ya Mbowe haina nia njema kwa Watanzania na ni lazima hatua zichukuliwe, vinginevyo taifa litaangamia.
Alisema wamechukizwa na kauli hiyo ya kibabe kwa kuwa inaweza kusababisha machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Tunalaani vikali kauli ya Mbowe kutaka nchi kuingia kwenye machafuko kwa kuitisha maandamano na migomo nchi nzima…ni kauli ya kihuni na haipaswi kuachwa ipite hivi hivi,” alisema.

CHADEMA DOM WAZIMWA
Polisi mkoani Dodoma imepiga marufuku maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika leo kuanzia viwanja vya Nyerere Square na kuishia Ofisi za Bunge.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula, alisema maandamano hayo ni batili na kuonya atayethubutu kuingia barabarani atakutana na sheria.
 “Chama hicho kimejipanga kufanya maandamano hayo katika wilaya zote za mkoa wetu, hii ni kinyume cha sheria na tunaonya wasijaribu na tumekataa,” alisema.
Alisema walipokea barua kutoka Ofisi ya CHADEMA kuomba kibali cha maandamano, ambayo yatadumu kwa saa mbili, lakini Polisi imeyapiga marufuku na kutangaza kuwa ulinzi zaidi utaimarishwa kukabiliana na yeyote.
Imeandikwa na Mariam Mziwanda, Furaha Omary, Mariam Zahoro na Happiness Mtweve, Dodoma.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru