Thursday 11 September 2014

Yona azidi kujitetea kortini


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, amekiri kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, aliagiza mchakato wa kumpata mkaguzi wa dhahabu usitishwe.
Akiendelea kutoa utetezi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana, Yona alidai kuwa hakutekeleza ushauri huo kwa kuwa Ikulu ilishatoa kibali cha kuendelea na mchakato.
Akiongozwa na wakili wake, Elisa Msuya, mbele ya jopo la majaji linaloongozwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Msajili Saul Kinemela, alidai Mei 2, 2003 aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, aliwaruhusu kuendelea na mchakato wa kumpata mkaguzi wa dhahabu, lakini alishauri serikali ichague mkandarasi atakayekuwa kama mtumishi wa serikali.
Barua hiyo ya Chenge, alidai, ilishauri mkandarasi huyo aajiriwe na kulipwa kwa mujibu wa kazi atakayokuwa akifanya na kuwa malipo yalipwe na serikali badala ya kampuni za madini.
Yona alidai aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, aliagiza Mei 15, 2003 kwamba mchakato wa kumpata mkaguzi huyo usitishwe.
“Nilimjibu Naibu Waziri kwa kumkumbusha kuwa alipokea maagizio ya Ikulu ya Mei 20, 2003. Sikutekeleza  agizo lake kwa sababu lilipitwa na maagizo ya Ikulu.
“Sikuwa na chaguo, nilifuata maagizo ya Ikulu ili mchakato uendelee na wote tuliopata dokezo la Ikulu tulifanya hivyo,” alidai.
Alidai kuwa alipokea mapendekezo kutoka kwa Mtaalamu wa Madini, Godwin Nyelo, yakitaka pia mchakato huo usitishwe wakati kamati ilikuwa ikiendelea.
“Tulitegemea Nyelo aende katika kamati kama mshauri na kuzikingia kifua hoja zake na wala si kurudisha majibu ya mapendekezo ya kusitisha mchakato.
“Nyelo alipendekeza kusitishwa kwa mchakato akidai malipo ya asilimia 1.9 ya mapatio ya dhahabu hayawezi kuiingizia kipato serikali,” aliongeza.
.
Mshtakiwa huyo alidai hakukaidi ushauri wa Nyelo isipokuwa aliuangalia akaona hautasaidia, akashauri arudi katika kamati.
Yona kutokana na muda aliishia hapo kujitetea. Jopo liliahirisha kesi hiyo hadi leo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali harasa ya sh bilioni 11.7.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja, walitenda makosa hayo Agosti, 2002 kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart Asseyers ya Uingereza kinyume cha sheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru