Thursday, 18 September 2014

Mawakili waomba kesi ya ugaidi ifutwe


NA MWANDISHI WETU
MAWAKILI wanaowatetea viongozi wa Jumuia ya Uamsho Zanzibar wameiomba mahakama kuiondoa hati ya mashitaka ya ugaidi dhidi  ya wateja wao.
Sheikh FArid Hadi Ahmed na wenzake,  wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama, kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi,  kukubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki vitendo.
Ombi hilo liliwasilishwa jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako ulinzi uliimarishwa kwa kuwepo askari wengi wakiwemo askari kanzu na mbwa wanne.
Wakili wa utetezi, Rajabu Abdallah kwa niaba ya jopo hilo, aliwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka kudai upelelezi haujakamilika.
Abdallah aliomba kuondolewa kwa hati hiyo, kutokana na kuwa na shaka kwamba mahakama hiyo si mahali sahihi pa kufunguliwa kesi hiyo.
“Nimeipitia hati ya mashitaka na nimeona shaka kuhusu kutuhumiwa kufanya makosa katika sehemu mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Kwa mujibu wa kifungu cha 244 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinatamka hatua za awali zitafanyika katika mahakama ya chini yenye mamlaka. Hati ya mashitaka haijaeleza eneo husika ambalo watuhumiwa wanadaiwa kufanya makosa,” alidai wakili huyo.
Alidai wanapata shaka iwapo mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa ilikuwa vyema iwapo hati hiyo ingekuwa imetaja eneo husika.
Aliomba hati hiyo iondelewe mahakamani hapo kwa sababu hati ya mashitaka imeshindwa kueleza sehemu husika.
Wakili Kweka alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani husikilizwa na Mahakama Kuu na kwamba hati imeletwa hapo kwa ajili ya washitakiwa kusomewa mashitaka, kuamriwa kwenda mahabusu, kuelezwa hatua ya upelelezi na kusomewa maelezo ya mashahidi upelelezi ukikamilika.
Alidai hati hiyo ipo sahihi mahakamani hapo na suala la kudai haipo sahihi linahitaji ushahidi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Hellen alisema atatoa uamuzi kuhusu maombi hayo Oktoba Mosi, mwaka huu. 
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sheikh Mselem Ali Mselem, Abdallah Said Ali au Madawa, Nassoro Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassani au Jibaba, Hussein Ally, Juma Sadala na Said Ally.
Pia wamo Hamis Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange au Mapala, Amir Juma, Kassim Nassoro, Salehe Juma na Jamal Noordin Swalehe.
hivyo. Wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Juni, 2013 na Julai, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Farid na Mselem wanadaiwa katika kipindi hicho huku akijua waliwaajiri Sadick na Farah ili kushiriki katika vitendo vya kigaidi.
Shitaka la nne linamkabili Sheikh Farid ambaye anadaiwa katika kipindi hicho aliwahifadhi watu hao, huku akijua kabisa kuwa walitenda vitendo hivyo. Mawakili wengine wanaowatetea washitakiwa hao ni Abubakar Salim, Ubaid Ahmed na Abdulfatar.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru