Wednesday, 3 September 2014

Wafanyabiashara wasitisha mgomo


NA WAANDISHI WETU
BIASHARA katika Jiji la Dar es Salaam, zimeanza kurejea kwenye hali yake ya kawaida baada ya juzi baadhi ya wafanyabiashara wa maduka kugoma na kuyafunga, wakipinga matumizi ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD).
Mgomo huo uliodumu kwa saa kadhaa, ulileta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali, hususan maeneo ya Kariakoo.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao walisitisha mgomo huo baada ya kufikiwa kwa maazimio katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa, ambacho kiliamuru maduka hayo kufunguliwa.
Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said  Mecky Sadiki, kiliazimia kufunguliwa kwa maduka hayo na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukutana na wafanyabishara hao ili kumaliza mgogoro huo.
Gazeti hili jana, lilishuhudia idadi kubwa ya maduka yakiwa yamefunguliwa, huku baadhi ya wanunuzi wa bidhaa mbalimbali katika maduka hayo wakiitaka TRA kufanya uhakiki katika maduka  kutokana na kuendelea kupatiwa risiti zisizokuwa za kielektroniki bila ya kupewa maelezo ya msingi.
Mmoja kati ya wanunuzi waliofika katika maduka hayo, Ngole Ramadhani, alisema inashangaza kuona bado utoaji wa risiti zisizokuwa za kielektroniki unaendelea wakati TRA ikiwasisitiza kutopokea risiti hizo kwa kuwa kufanya hivyo ni ukwepaji wa kodi.
Alisema ni vyema kwa wafanyabishara hao kukutana na TRA ili kuondoa tofauti zao na kuiwezesha serikali kukusanya kodi kwa maendeleo ya taifa na kulinda maslahi ya pande zote husika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mgomo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alisema kimsingi wanakubaliana na matumizi ya mashine hizo huku akitoa angalizo kwa TRA kurekebisha baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye mashine hizo.
Aliongeza kuwa mfumo wa EFD kutambua manunuzi pekee bila kuhifadhi kumbukumbu ya matumizi na gharama nyingine za uendeshaji wa biashara ni vyema ukaangaliwa upya, kutokana na kuwasababishia hasara.
Minja alisema kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, wanatarajia kukutana na Kamishna Mkuu wa TRA ili kujadili kuhusiana na malalamiko yao.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema msimamo wa mamlaka hiyo ni kuwataka wafanyabiashara hao kuzingatia taratibu za kisheria na kutumia mashine hizo.
Alisema operesheni ya kukagua na kuhakiki matumizi ya mashine hizo, itaendelea kama kawaida.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru