NA ALLY NDOTA, ZANZIBAR
KATIBU wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), Zanzibar wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, amewataka wana CCM kutoendeleza makundi kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha nguvu za Chama hicho.
Alisema viongozi wa CCM katika majimbo yote visiwani hapa, waache kuendeleza makundi yaliyotokana na uchaguzi uliopita, badala yake waelekeze nguvu katika kusimamia sera na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kuwaletea maisha bora wananchi.
Alisema dhamira ya CCM ni kuhakikisha majimbo yote yaliyochukuliwa na upinzani yanarejeshwa na kwamba, wakati wa maandalizi ni sasa.
“CCM ni Chama kikubwa, chenye nguvu kisiasa na kujipatia heshima na umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania, hivyo viongozi hawapaswi kufanya mambo ambayo yatapunguza kama si kumaliza kabisa haiba nzuri ya CCM mbele ya walimwengu,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi wa majimbo ya Mtoni na Magogoni, umuhimu wa kudumisha mshikamano na umoja baina yao na wanachama ili kutekeleza kikamilifu majukumu yao.
Akizungumzia tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji wa Chama kuwabeba wanachama wanaotangaza nia ya kuwania urais, ubunge na uwakilishi katika uchaguzi ujao, aliwataka kuacha mara moja kwani ni kukiuka kanuni, miongozo na taratibu za Chama.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru