NA PETER KATULANDA, MAGU
MWENYEKITI wa CCM Kata ya Mwamanyili wilayani Busega, Simiyu, Ramadhani Msoka na wenzake watano, wamepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji.
Washitakiwa hao akiwemo Mshauri wa Mahakama ya Mwanzo ya Nyashimo wilayani humo, Libent Rwegarulila, ambaye ni mshitakiwa namba moja, walisomewa mashitaka hayo juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Magu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Robert Masige.
Awali, Msoka na wenzake watatu walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo, Agost 29, mwaka huu na kusomewa mashitaka hayo bila ya watuhumiwa wenzao wawili, Yela Magubu na Lupoja Mbeyo (ambao sasa ni washitakiwa namba tatu na nne, kukamatwa na kuunganishwa.
Washitakiwa wengine wa awali katika kesi hiyo namba 126/2014 ni Meshack Samson (ambaye ni mshitakiwa namba mbili) na Kubin Nkondo ambaye (mshitakiwa wa sita), ambapo Msoka sasa ni mshitakiwa wa tano.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Edward Mokiwa, alidai washitakiwa walitenda makosa hayo Agosti 23, mwaka huu, saa 7 usiku katika eneo la Nassa Ginnery wilayani Busega.
Alidai siku ya tukio washitakiwa wakiwa na silaha za jadi walimvamia Mwalimu Samuel Mkumbo na kuporac sh. milioni 18 kisha kundi hilo kumbaka kwa zamu mpangaji wa mwalimu huyo (jina linahifadhiwa) ambaye pia ni Mwalimu.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo. Hata hivyo, walidai kuwa kesi hiyo ni ya kisiasa na wamesingiziwa. Madai hayo yalipingwa na Mokiwa, ambaye aliieleza mahakama kuwa mashitaka ya unyang’anyi na ubakaji si ya kisiasa.
Upepelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na washitakiwa wote wako rumande kutokana na Hakimu Masige kusema mashitaka hayo hayana dhamana chini ya kifungu namba 148, kifungu kidogo cha 5 a (1). Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 24, mwaka huu.
Thursday, 11 September 2014
Watano kortini kwa tuhuma za ubakaji
02:28
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru