NA WILLIAM SHECHAMBO
MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama na waandishi wa habari nchini kushirikiana katika majukumu yao ya kazi ili kulinda amani ya nchi.
Pia amezitaka taasisi hizo kuzingatia mipaka yao na katika utendaji ili kuepuka migongano au chuki zinazoweza kutokea wakati wa kutimiza wajibu wao kazini.
Alitoa wito hiyo katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, jana, alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano kati ya vyombo vya habari, ulinzi, usalama na sheria ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Vyombo vya ulinzi mnapaswa kujua kwamba waandishi wa habari si maadui zenu…mnaweza kukaa nao vizuri,” alisema.
Washiriki wa mkutano huo walitakiwa kutambua kazi zao na kuhakikisha wanatekeleza majukumu , kuepusha migogoro hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.
Makamu wa Rais alisema mkutano huo wa kwanza wa kihistoria kuwakutanisha watendaji hao, umekuja wakati mwafaka kutokana na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la vyombo vya habari, huku jamii nayo ikiwa na shauku ya kusambaza habari kadri iwezavyo.
Alisema waandishi wanapaswa kudhibiti usambaaji wa habari zisizotakiwa kusambaa kwa maslahi ya ulinzi na usalama wa nchi kwa sababu sheria zilizoko hazina nguvu tena ya kufanya hivyo.
“Habari nyingine zinaweza kusababisha chuki na kuchochea vurugu, hivyo pande hizo zinapaswa kushirikiana katika kutetea maslahi ya taifa na amani kwa wananchi,” alisema.
Alivishauri vyombo vya habari kujenga taswira chanya kwa vyombo vya ulinzi na usalama huku akivitaka vyombo hivyo navyo, kutoa ushirikiano wa dhati kwa wanahabari.
“Kila upande una mipaka yake ya kiutednaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku… kinachotakiwa ni kuelewana kwani nia na jukumu lenu nyote ni kulinda amani,” alisema.
Kupitia mkutano huo, alisema ni vema vyombo hivyo vikafungua ukurasa mpya wa mawasiliano.
Pia Dk. Bilal alivitaka vyombo vya habari kuanza mfumo wa kuwa na waandishi wataalam wa maeneo mbalimbali ikiwemo uandishi wa habari za mafuta na gesi.
“Wananchi wanapaswa kujua mambo haya vizuri, pia masuala ya afya, ukimwi, lazima kuwe na waandishi wataalam,” alisema.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Habari Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, alisema mkutano huo ni zao la mpango mkakati ulioandaliwa na MCT kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Naye Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga, Mtendaji wa MCT, sababu kubwa ya kuandaa mkutano huo ilichangiwa na tukio lililoleta hofu ya usalama nchini, pale ambapo mwandishi wa habari Daudi Mwangosi alipouawa na vyombo vya usalama wakati akitekeleza majukumu yake mkoani Iringa.
Alisema baada ya tukio hilo, uaminifu kati ya wanahabari na wanausalama ulipungua, hali ambayo haina tija kwa maendeleo ya taifa.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo, Joseph Kulangwa, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, alieleza kufurahishwa na kauli ya Dk. Bilal na kusema imetoa mwongozo wa kufikia malengo ya mkutano.
Alisema wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu baadaye mwakani, suala la amani na mshikamano ni muhimu.
Hoja zilizojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuhusiana na usalama wa mwanahabari, utawala na sheria, uandishi wa habari za uchunguzi, mazingira na uzoefu pamoja na uwezekano wa vyombo vya usalama kuchangia uhuru wa kujielewa.
Hata hivyo jeshi la polisi halikutuma mwakilishi yeyote katika mkutano huo, licha ya kwamba, ratiba ilionyesha ofisa mmoja wa jeshi hilo kuwasilisha mada.
Wednesday, 17 September 2014
Dk. Bilal avipasha vyombo vya ulinzi na usalama, waandishi wa habari
07:39
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru