Tuesday, 9 September 2014

Kivuko kipya cha Mv Dar kuwasili nchini mwezi ujao

NA MUSSA YUSUPH
SERIKALI imetangaza kukamilika kwa ujenzi wa Kivuko kipya cha Mv Dar es Salaam,
kitakachokuwa na uwezo wa kuvusha watu zaidi ya 300 kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.
Kukamilika kwa kivuko hicho, kinachotarajiwa kuwasili nchini katika kipindi cha wiki tatu zijazo,kunatokana na jitihada za serikali katika kupunguza msongamano wa magari na shida ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Mbali na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya abiria, kivuko hicho pia kitakuwa na kasi itakayowezesha kufanya safari zake haraka zaidi, kuliko vivuko vingine vilivyopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema Kivuko hicho kilichoigharimu serikali sh. bilioni 7.9, kinatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Bagamoyo na Dar es Salaam kwa kufanikisha shughuli za kibiashara kati ya pande hizo kwa haraka zaidi.
Aliongeza kuwa tayari mkandarasi kutoka nchini Denmark ameshaanza utaratibu wa kukisafirisha kuja Dar es Salaam, hivyo wananchi wategemee kuanza kufanya kazi mara tu baada ya kuwasili kwake.
Wakati huo huo, Waziri Magufuli amezindua kivuko cha Mv Kigamboni kilichokuwa kikifanyiwa ukarabati na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kamandi ya Wanamaji.
Katika uzinduzi huo, Magufuli alilipongeza jeshi hilo kwa kukamilisha ukarabati wake kwa haraka zaidi na kuokoa zaidi ya nusu ya fedha iliyokuwa ikitarajiwa kutumika katika ukarabati huo kama ungefanyika nje ya nchi.
Alisema awali, serikali ilitaka kukipeleka kivuko hicho Mombasa, Kenya kwa ukarabati, lakini kutokana na uwezo wa juu walionao wahandisi kutoka JWTZ, ndicho kilichoisukuma kulipatia jeshi hilo kazi ya ukarabati.
Aidha, ili kuepukana na tatizo la kupungua kwa kina cha maji, Waziri Magufuli aliliomba jeshi hilo kuhakikisha ifikapo kesho jioni, kivuko hicho kinaingizwa baharini na kuanza kuhudumia wananchi, ombi ambalo lilikubaliwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kamandi ya Wanamaji, Brigedia Jenerali, Rogastian Laswai, alisema jeshi limefanya kazi kwa uzalendo na idadi kubwa ya vifaa walivyotumia katika ukarabati huo ni vya kutoka nchini.
Alisema wamefanikiwa kuokoa fedha za kigeni, ambazo zingetumika kununua baadhi ya vifaa na kuwalipa wahandisi kutoka nje ya nchi na wamehakikisha usalama wa kivuko unabakia katika mikono ya Watanzania licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru