Tuesday, 23 September 2014

CCM yahofu uchaguzi mkuu 2015 kuvurugika

Na Suleiman Jongo, Chalinze

Nape Nnauye
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuna uwekezano wa Uchaguzi Mkuu wa mwakani kuvurugika kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kulazimisha matumizi ya mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR).
Kimesema mfumo huo utaigharimu serikali mabilioni ya shilingi na kwamba, unaweza usitoe mafanikio yenye tija kama inavyotarajiwa kwa kuwa tayari umetoa matokeo mabaya kwenye baadhi ya nchi zilizoanza kuutumia.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana kuwa mfumo huo unaweza kuleta matatizo makubwa katika uchaguzi, lakini NEC imekuwa ikishinikiza kutumika kwa lengo la kutengeneza ulaji.
Kiasi cha sh. bilioni 290 kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kufungwa kwa miundombinu ya kuwezesha mfumo huo kutumika na kwamba, umegubikwa na usiri mkubwa nyuma yake.

“Huu mfumo una siri kubwa nyuma yake.Mbali na hofu ya kuvuruga uchaguzi, lakini ni matumizi mabaya ya fedha za umma zinazotaka kutafunwa na wajanja wachache kwa maslahi yao binafsi,” alisema Nape.
NEC imetangaza kuanza kutumika kwa mfumo huo wa BVR katika uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kuandikisha upya daftari la wapigakura.
Nape alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Chalinze mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Alisema mfumo huo unazua maswali mengi yasiyo na majibu huku baya zaidi ikiwa ni historia ya BVR katika nchi mbalimbali, zikiwemo za Malawi na Kenya ambazo zililazimika kuacha kuutumia licha ya kutumia fedha nyingi.

“Nchi zote zilizotumia mfumo huo ziliingia kwenye matatizo. Mfano mzuri ni Kenya, ambao walilazimika kuuacha hatua za mwisho huku mabilioni ya fedha yakiwa yameingia mifukoni mwa wajanja.
“BVR itazusha maswali mengi katika uchaguzi mkuu mwakani. Uchaguzi ukivurugika, lawama zitakuja kwa CCM kwamba tulikuwa tunataka kuchakachua matokeo. Hatukubaliani na hilo na hatuko tayari kuona likitokea,” alisema Nape.
Mbali na kuvuruga uchaguzi, Nape alisema mfumo huo pia utaigharimu nchi mabilioni ya fedha za umma zinazoweza kutumika kuhudumia sekta zingine za kijamii ili kuwaletea Watanzania maendeleo.

“Inaonekana wajanja wachache wanataka kuitumia NEC kutengeneza mazingira ya ulaji wa fedha za umma. Sidhani kama nia yao ni kuboresha mfumo wa kupiga kura bali kuvuruga kama ilivyotokea kwenye nchi zingine,” aliongeza.
Nape alisema badala ya NEC kutumia mabilioni hayo, ilipaswa kukaa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kutumia taarifa zake kuboresha daftari la kupigia kura.
Kwa mujibu wa Nape, NEC ikishirikiana na NIDA watapunguza gharama hizo kwa kuwa katika zama hizi za sayansi na teknolojia, NEC itapata kila wanachokitaka kupitia NIDA, zikiwemo taarifa za wapiga kura.
Aliitaka NEC kujifunza kwenye nchi zingine zilizotumia mfumo huo na kushindwa kusaidia uchaguzi, badala yake kuibua vurugu.

“NEC iwe na huruma na fedha za Watanzania kwani kwa teknolojia ya sasa, nchi nyingi zinatumia kadi moja kupata taarifa mbalimbali, ikiwemo upigaji kura,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru