Wednesday 3 September 2014

Asomewa mashitaka wodini


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, jana ilihamia katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, kwa ajili ya kusomewa mashitaka mtuhumiwa Abdulkarim Thabit Hasia anayedaiwa kufanya uwakala wa kusajili vijana kujiunga na kundi la Al Shabaab.
Hasia ambaye amelazwa katika hospitali hiyo kwa takriban miezi minne, ilikuwa asomewe mashitaka na kuunganishwa na wenzake, Mei mwaka huu lakini ilishindikana kutokana na kutokuwa na fahamu.
Mshitakiwa huyo alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali Augustino Kombe, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mustapher Siyani, akiwa katika wodi Grade One.
Kabla ya kusomewa mashitaka, Hakimu Siyani alimweleza mshitakiwa kwamba anaunganishwa katika kesi inayowakabili watu 11 ambao walishafikishwa mahakamani.
“Nimekuja ili usomewe mashitaka yako, kwani mara ya kwanza nilikuja Mei, mwaka huu, lakini hakuwa na fahamu. Tumeamua kuja leo (jana) kwa kuwa unaelewa kinachozungumzwa na baada ya kusomewa utakuwa chini ya uangalizi wa askari magereza,” alisema Hakimu Siyani.
Pia alimwarifu mshitakiwa kwamba hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Kombe alimsomea  mshitakiwa mashitaka 16 ya ugaidi na kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, kwa kutajwa.
Hata hivyo, waandishi wa habari walikutana na vizingiti vya kuzuiwa kupiga picha na askari aliyekuwepo wodini na kutakiwa wawasiliane na polisi, ambao nao waliwataka kuwasiliana na uongozi wa hospitali.
Waandishi walipowasiliana na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Josian Mlay, naye alirusha mpira kwa wauguzi wa wodini na kudai wao ndio wenye idhini ya kutoa kibali cha mgonjwa kupigwa picha.
Kwa upande wao, wauguzi nao walidai hawana mamlaka bali mwenye ridhaa ni mgonjwa mwenyewe.
Kesi hiyo imeahairishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, itakapotajwa tena na washitakiwa wako mahabusu.
Kabla ya mahakama kuhamia hospitalini hapo, washitakiwa wengine katika kesi hiyo, walilalamika mbele ya Hakimu Siyani juu ya ndugu zao kuzuiwa kuingia kufuatilia kesi mahakamani.
Pia walidai mshitakiwa mwezao ambaye yuko hospitalini alikuwa mzima hadi siku anakamatwa na sasa amekatwa mguu kutokana na mateso ya polisi.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Siyani alisema mahakama haijazuia ndugu zao kufika kusikiliza kesi hiyo na kusema tarehe zijazo wafike mahakamani na hakuna haja ya kuzuiwa.
Kuhusu madai ya mwenzao kukatwa mguu, Hakimu Siyani alisema kila mshitakiwa anatakiwa awasilishe malalamiko yake na si kumsemea mwenzake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru