Thursday, 11 September 2014

Mwigulu awavaa waajiri  • Aagiza wakamatwe na kushitakiwa haraka

NA MOHAMMED ISSA NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SERIKALI imeagiza kushitakiwa kwa waajiri wote nchini, ambao hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Pia imewaonya waajiri kuacha mara moja tabia ya kutopeleka ama kuchelewesha michango ya wafanyakazi kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Mbali na hilo, imesema inaridhishwa na utendaji unaofanywa na uongozi wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, kwa kuongeza thamani ya mfuko huo.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa 24 wa wanachama na wadau wa mfuko wa PPF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Alisema waajiri ambao hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, wasifumbiwe macho na kwamba washitakiwe kwa mujibu wa sheria.
Mwigulu alisema katika miaka ya hivi karibuni, kumetokea tabia ya baadhi ya waajiri kuchelewesha ama kutopeleka michango ya wafanyakazi kwenye mifuko hiyo kinyume cha sheria.
Alisema ni kosa kisheria kwa mwajiri kuchelewesha ama kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wanaofanya hivyo, wachukuliwe hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kushitakiwa.
”Waajiri ambao hawawasilishi michango ya watumishi wao, wasionewe huruma, washitakiwe kwa mujibu ya sheria,” alisema.
Aliwataka baadhi ya waajiri kuacha tabia ya kusubiri wafanyakazi mpaka wanapostaafu ndio wawapelekee michango yao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali imeunda kamati kwa ajili ya kuhakiki madeni inayodaiwa na PPF ili iweze kulipa.
Alisema madeni hayo yakianza kulipwa, mfuko mfuko unaweza kuliendeleza taifa kwenye miundombinu mbalimbali.
Mwigulu alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina mchango mkubwa kwa jamii na kwamba asilimia 12 ya uchumi wa taifa, unatokana na mifuko hiyo.
Alisema wakati umefika sasa, PPF kutoa mikopo kwa ‘saccos’ ambazo si za mfuko huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, alisema kauli mbiu ya mkutano huo ni Hifadhi ya Jamii Chachu ya Maendeleo ya Kijamii.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru