Na Rodrick Makundi, Moshi
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Philemon Luhanjo, alitangaza hatua hiyo juzi mjini hapa, mbele ya viongozi wa serikali mkoa wa Kilimanjaro, uongozi na watumishi wa MUCCoBS.
Baada ya kupandishwa hadhi chuo hicho, sasa kitaitwa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, kikiwa chini ya baraza la mpito linaloongozwa na Mwenyekiti, Profesa Gerald Monela, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa SUA.
Akitangaza mabadiliko hayo, Luhanjo,ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, alisema chuo hicho kimepandishwa hadhi kuanzia Julai 3, mwaka huu, baada ya kufanyiwa tathmini na vyombo vya usimamizi wa taasisi za elimu ya juu nchini, ikiwemo tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kwa mujibu wa Luhanjo, mabadiliko hayo pia yameambatana na uteuzi uliofanywa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa wa viongozi wa muda na vyombo vya uamuzi kwa kipindi cha mpito.
Mbali ya Profesa Monela kuwa mwenyekiti wa baraza, pia iliyokuwa bodi ya uongozi ya MUCCoBS na kamati zake, zimekuwa baraza la mpito mpaka litakapoundwa baraza kamili.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa mkuu wa chuo cha MUCCoBS, Profesa Faustine Bee, ameteuliwa kuwa kaimu makamu mkuu wa chuo, akisaidiwa na Basil Liheta, anayekuwa Kaimu Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) na Ndayizera Manta, anayekuwa Kaimu Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo (Utawala).
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru