Thursday, 11 September 2014

‘Kifaru’ cha JWTZ chavamia nyumba


  • Watatu wafariki papo hapo, wamo wanajeshi
  • Wengine taabani hospitali, JWTZ yachunguza

Na Rashid Mussa, Mtwara
WATU watatu wakiwemo askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia baada ya gari maalumu la kubebea askari la jeshi hilo kugonga nyumba katika Kijiji cha Mnollela mkoani Lindi.
Katika ajali hiyo iliyotokea jana alfajiri wakati gari hilo likitokea Mtwara kwenda Masasi, askari wengine sita walijeruhiwa huku wawili kati yao wakiwa na hali mbaya.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi, Renata Mzinga, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kutaja namba za gari hilo kuwa ni 018APC la kikosi cha Reget, lililokuwa likisendeshwa na askari wa JWTZ, Shadhil Nandonde (28).
Alisema gari hilo liliacha njia na kugonga nyumba mbili katika kijiji hicho na kusababisha kifo cha raia mmoja na askari hao wawili.
Renata aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni mkazi wa kijiji hicho, aliyekuwa katika nyumba moja kati ya mbili zilizogongwa, Someye Kamteule (75) na askari namba MT 10728 Pascal Komba (23) aliyekuwa katika gari hilo.
Alisema askari mwingine alikufa wakati akipata matibabu katika hospitali ya mkoa wa Mtwara ya  Ligulla, na kufanya idadi ya waliyokufa katika ajali hiyo ya aina yake  kufikia watatu.
Mwingine ni askari namba MT. 106842 Feruzi Haji (22), ambaye alifariki baada ya kufikishwa hospitali ya Ligula kupatiwa matibabu.
Kamanda Renata aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  askari namba MT 99018 Mbaruku Duchi (28), ambaye hali yake ilikuwa mbaya, MT. 10744 Simon Edward (23), MT. 1077263 Omari Makao, MT, 107442, Simon Maselle (23) na MT107218 Ndekenya (22) na dereva Nandonde.
=Akizungumzia ajali hiyo, Mganga Mfawadhi wa Hospitali ya Ligula, Lobi Kissambu, alisema kati ya majeruhi wawili walipokelewa wakiwa katika hali mbaya, mmoja wao Feruzi alikufa wwakati  akipatiwa matibabu.
Alisema Duchi alihamishiwa katika Hospitali ya Misheni Nyangao iliyoko mkoani Lindi kwa matibabu zaidi na wengine waliolazwa wodi namba nane hali zao zilikuwa zinaendelea vizuri.
Kutokana na ajali hiyo, JWTZ imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali  hiyo iliyosababisha vifo vya askari waliokuwa katika msafara wa kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Makao Makuu ya JWTZ, askari hao walikuwa wakitumia magari maalumu ya kubeba askari.
Taarifa hiyo ilisema JWTZ imeungana na familia za marehemu katika kuomboleza vifo vya askari hao pamoja na raia.
Pia JWTZ inafanya uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo kwa kushirikiana na  polisi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru