Tuesday, 2 September 2014

Mbaroni kwa kujifanya Ofisa Usalama wa Taifa


NA EMMANUEL MOHAMED
MKAZI wa Kinyerezi, Dar es Salaam, Saimon Meena, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kujifanya Ofisa Usalama wa Taifa.

Suleiman Kova
Hatua hiyo ya Meena (40), ililenga kumwezesha kufanya utapeli ili kujipatia sh. milioni 25 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Somalia.
Meena, maarufu kwa jina la Gunner, anadaiwa kuwatisha baadhi ya wafanyabiashara jijini Dar es Saalam kuwa wanahusika na matukio ya kigaidi hivyo kuhatarisha usalama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Kanda Maalumu, Suleiman Kova, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisakwa kwa muda mrefu kuhusiana na matukio ya utapeli.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mtuhumiwa huyo si mtumishi wa Idara ya Usalama na kwamba, amekuwa akitumia wadhifa huo kufanya uhalifu.
“Huyu tulikuwa tunamsaka kwa muda mrefu, sasa tumemnasa, alijaribu kumtapeli mfanyabiashara Abdi Mohamed na kutaka apewe sh. milioni 25,” alisema Kamishna Kova.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru