NA MWANDISHI WETU, MUFINDI
HALMASHAURI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mufindi, imewataka viongozi wa matawi na kata kutokubali kuwabeba baadhi ya wanachama walioanza kujipitisha kwenye majimbo, kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Katibu wa CCM wilayani Mufindi, Miraji Mtaturu, alisema hayo wakati akisoma maazimio ya halmashauri hiyo, iliyokuwa na lengo la kupokea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.
Alisema ni kosa kikanuni kuanza kujipitisha wakati ambao chama kinatakiwa kufanya kazi za maendeleo kwa kushirikiana na viongozi waliopo madarakani.
Aliwataka viongozi wa kata na matawi kutokubali kuwabeba, wala kuwaruhusu watu wa aina hiyo, kwa madai kuwa wanadhoofisha utendaji wa kazi wa viongozi waliopo madarakani.
Mtaturu aliahidi hatua kali za kikanuni zitachukuliwa dhidi ya wanaojipitisha na wanachama wanaowapokea.
Alisema moja ya adhabu inayoweza kutolewa kwa viongozi hao ni pamoja na kuenguliwa uongozi.
Wabunge wa majimbo ya wilaya ya Mufindi ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa wa Mufindi Kaskazini na Mendrad Kigola wa wa Mufindi Kusini.
Awali, Mkuu wa wilaya hiyo, Evarista Kalalu, alisema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unaendelea vizuri kiasi cha kuondoa malalamiko ya wananchi katika sekta mbali mbali, ikiwemo maji na elimu.
Alisema upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo bado sio mzuri, kwani umeongezeka kwa kiasi kidogo, kutoka asilimia 61.5 hadi 63 mjini na asilimia 61.6 hadi 62 vijijini.
Wednesday, 10 September 2014
‘Msiwabebe wanaojipitisha majimboni’
03:43
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru