Tuesday, 23 September 2014

‘Serikali isambaze teknolojia ya usindikaji mazao’

Na Nathaniel Limu, Manyoni
SERIKALI imetakiwa  kushirikiana na wadau katika kusambaza teknolojia ya usindikaji wa mazao ya kilimo kwa wananchi na kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa na zana za kisasa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,  Andreas Whero, aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano  kwa wajasiriamali juu ya  teknolojia ya usindikaji mazao ya matunda, vinywaji na vyakula.
 Whero alisema  wakati huu ambapo kuna changamoto kubwa ya uzalishaji wa bidhaa zinazohimili ushindani kitaifa na kimataifa,  kuna haja kubwa ya wakulima  na wajasiriamali kufikiwa na teknoloji ya usindikaji wa vyakula.
 Alisema lengo ni kuhakikisha  bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima mashambani, zinaongezwa thamani kwa kusindikwa na kufungashwa vizuri, ili zisiharibike.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema kuna changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi na serikali.
Changamoto hizo walizitaja kuwa ni ukosefu wa zana na vifaa kwa ajili ya usindikaji vijiji, ukosefu wa nishati ya umeme na dawa ya kuzuia mazao kuoza.
Walisema bidhaa za vyakula, vinywaji na matunda, zinazosindikwa kwa teknolojia   ya kisasa, zinaweza kudumu kwa zaidi ya miezi sita bila kuharibika wala kupoteza ubora wake.
Mafunzo hayo  yaliandaliwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na VETA kanda ya kati.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru