Tuesday, 9 September 2014

JK, TCD watoa mwelekeo mpya  • Bunge la Katiba kuendelea, UKAWA waridhia
  • Katiba iliyopo kuboreshwa kwa uchaguzi ujao

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
KIKAO baina ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimetoa mwelekeo mpya katika mchakato wa Katiba Mpya.
Mwelekeo huo ni matunda ya vikao viwili, ambavyo Rais Kikwete alivifanya na vyama wanachama wa TCD, kwa ajili ya kujadili changamoto za Bunge Maalumu la Katiba, baada ya baadhi ya vyama kususia vikao vya bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma.
Katika kikao hicho, TCD imebariki kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na kwamba, haliwezi kusitishwa kama ilivyokuwa ikipendekezwa na wachache.
Pia imependekezwa kufanyika kwa mabadiliko madogo kwenye Katiba ya sasa ili kuiwezesha kuendelea kutumika katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Kituo hicho kinaundwa na vyama vya siasa vyenye wabunge bungeni, ambavyo ni CCM, CUF, NCCR-MAGEUZI, TLP, CHADEMA, UDP, UPDP, ambapo wenyeviti wake na makatibu wakuu walihudhuria.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, Bunge litaendelea na vikao vyake hadi litakapokamilisha kazi yake Oktoba 4, mwaka huu.
‘’Wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuwa hatua hii ya mchakato wa Katiba iendelee hadi Oktoba 4, mwaka huu, ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa kupatikana,’’ alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na bunge hilo, Katiba inayotafutwa haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu mwakani kutokana na muda kutokidhi kukamilisha kazi hiyo.
Cheyo alisema kwa mujibu wa mchakato huo, kura ya maoni itakayopigwa na Watanzania inatarajiwa kufanyika mwezi Aprili, mwakani.
Alisema iwapo kura hiyo italazimika kurudiwa, kazi hiyo inaweza kufanyika Juni au Julai, mwakani, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa kuvunjwa kwa ajili ya Uchaguzi  Mkuu.
“Kama tutalazimisha Katiba Mpya itumike kwenye uchaguzi mkuu mwakani, itatulazimu kuongeza uhai wa Bunge na serikali kwa zaidi ya mwaka, jambo ambalo haliwezekani,” alisema Cheyo.
Aliongeza kuwa wamekubaliana kurekebishwa kwa baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye katiba ya sasa, ikiwemo kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itasimamia uchaguzi na mshindi wa Urais ni lazima ashinde kwa zaidi ya asilimia 50.
Mapendekezo mengine ni kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika uchaguzi.
Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyama vingine vya siasa,  ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine katika Katiba, kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliopangwa ni mdogo.
‘’TCD kwa kupitia vikao vyake, itaratibu, itajadili mapendekezo hayo na kuyapeleka serikalini kwa hatua zaidi kwa kuwa muda tulionao ni mdogo na mabadiliko hayo yatajadiliwa kwenye Bunge la Novemba, mwaka huu na ikitokea tukichelewa basi hadi Februari mwakani,’’ alisema na kutumia fursa hiyo kumpongeza Rais Kikwete kwa usikivu wake na kukubali ombi la kukutana na TCD.
 ‘’Tunataka nchi iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia, yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na uchaguzi huru na wa haki,’’ alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema tangazo la rais linalitaka Bunge hilo kukamilisha kazi zake ifikapo Oktoba 4, mwaka huu.
Hata hivyo, Hamad alisema Bunge hilo limesha andika barua kwenda serikalini ili kuomba siku za mapumziko zitolewe na kuongezwa katika siku za kazi.
Alisema ni mategemeo yake kuwa Bunge hilo litafanya kazi yake iliyotumwa ya kutoa katiba pendekezi.
‘’Suala la kutumika au kutotumika kwa Katiba katika uchaguzi mkuu ujao si kazi ya Bunge hili, tumepewa kazi ya kutunga Katiba pendekezi na hapo itakuwa mwisho wa kazi yetu ya Bunge Maalumu,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru