Wednesday, 10 September 2014

DC Iringa awaasa wanaoishi na VVU


NA TUMAINI MSOWOYA, IRINGA
MKUU wa wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba, amewataka wananchi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi  (VVU), kutokata tamaa, badala yake wafuate masharti ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Alitoa wito huo wakati Shirika la  Utafiti wa Tiba na Afya Barani Afrika, (AMREF),  lilipokuwa likitoa msaada wa baiskeli 50 kwa vikundi 17 kati ya 36 vya watoto salama, vinavyoundwa na wanawake wenye  VVU,  Iringa Vijijini.
Alisema kuishi na VVU sio mwisho wa maisha, kinachotakiwa ni kutokata tamaa na kufuata ushauri wa madaktari.
Aidha aliwapongeza wanawake hao kwa kujishughulisha na ujasiriamali na kutunza familia zao. Alisema jambo hilo ni mfano wa kuigwa.
Aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kupima afya zao ili kujua kama wameambukizwa au la.
Mmoja wa  mama mwenye maambukizi, Kalista  Haule, kutoka kijiji cha Migori, alisema wameamua kuvunja ukimya ili kuwasaidia wanaoogopa kupima, wajitokeze kujua afya zao.
Alilishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada wa baiskeli, jambo ambalo litawasaidia kwenye shughuli za kiuchumi.
 Aliwashangaa baadhi ya Watanzania wanaoendelea kuwacheka au kuwasimanga wenye maambukizi ya VVU.
Kwa upande wake, Thadei Madege wa kijiji cha Kihanga,  alisema baiskeli walizopewa zitawasaidia katika safari zao za kufuata dawa katika vituo vya afya, pamoja na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Pudenciana Kisaka, alisema vikundi hivyo vinasaidia kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na  wanawake wenye maambukizi hayo kuzingatia ushauri ili wanapopata mimba wajifungue watoto wasio na maambukizi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru