Tuesday 9 September 2014

Pinda awataka wanasheria wawe wazalendo


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka wanasheria kutoka nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, waweke mbele maslahi ya wananchi wa kawaida wakati wanapoingia mikataba na wawekezaji kwenye sekta ya madini.
Alitoa wito huo jana wakati akifungua semina ya siku tano juu ya mafunzo ya kuingia makubaliano na mikataba kwenye sekta ya madini kwa wanasheria wa sekta ya umma kutoka nchi wanachama wa Jumuia hiyo ulioanza leo kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na washiriki wa mkutano huo kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania, Pinda alisema wanapaswa wawajali sana wananchi walio maskini kwa sababu wao hawana fursa ya kuingia kwenye vikao kama vyao na kutoa sauti juu ya kile wanachokitaka.
“Muwapo ofisini kwenu au kwenye miji yenu mikuu, mnapojadiliana na wawekezaji na kufikia makubaliano kuhusu rasilimali za nchi, siku zote muwafikirie hawa watu wa chini, walio maskini ambao ni wengi na wako nje ya majengo yenu.
“Wao ndiyo wadau wakuu, lakini hawana uwezo wa kuingia kwenye vikao kama hivi. Sote tunatambua kwamba wameishi na hizo rasilmali kwa vizazi vingi tu. Licha ya umaskini wao, wanaishi juu ya ardhi ambayo chini yake kuna utajiri tele wa madini na rasilimali nyingine.  Ninawasihi sana muwafikirie watu hawa kabla ya kufanya maamuzi yoyote,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema ili jambo hilo liweze kufanikiwa, ni lazima wanasheria kama wadau wa mwanzo kabisa, wawe tayari kukataa kupokea fedha chafu na vishawishi kutoka kwa wawekezaji na siku zote waweke uzalendo mbele kwa maslahi ya nchi zao.
“Rasilimali za bara la Afrika hazijaleta maendeleo kwa wakazi wa bara hili kwa sababu wanaofaidika ni makampuni makubwa kutoka nje na watu wachache sana wenye nafasi huku walio wengi wakiambulia patupu. Ni theluthi moja tu ya mikataba ya uchimbaji madini inayolifaidisha bara zima la Afrika, ikilinganishwa na faida ambayo bara la Amerika Kusini inanufaika nayo,” alisema.
Ili kuepukana na hali hiyo, Waziri Mkuu alisema umefika wakati wa kukataa kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za kimataifa na kuhakikisha kuwa kampuni hizo zinalipa kodi katika kila nchi husika ya Afrika Mashariki.
“Natumaini hii semina itasaidia kutufungua macho katika maeneo ambayo mikataba yetu na sheria zetu zilikuwa zinalegalega, ili kuanzia sasa tuweze kunufaika na rasilimali zetu,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda alisema umefika wakati wa kuhakikisha serikali za nchi husika zinaweka sera madhubuti na miongozo ya kisheria itakayohakikisha mikataba inayoandaliwa kwa ajili ya utafutaji na uendelezaji wa madini na rasilimali zake inazinufaisha nchi kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema semina hiyo ni muhimu kwa sababu wanaolengwa ni wanasheria kutoka Afrika Mashariki na Afrika ndilo eneo pekee lenye rasilmali ambazo bado hazijaendelezwa.
“Wanapaswa kutambua kwamba mfanyabiashara yeyote akija ni lazima anatafuta faida. Na ukilala tu, yeye anapata faida kubwa sana. Wakienda kusaini mikataba, hawa wanasheria wanapaswa kuangalia sheria za nchi husika, lakini pia wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuacha tamaa. Wanatakiwa wafanye maamuzi kwa niaba ya wananchi,” alisema.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema sekta ya madini ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa haraka hapa nchini, lakini inachangia chini ya asilimia moja ya ajira zote.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru