Tuesday, 23 September 2014

Serikali yapania kutokomeza utapiamlo

NA SOPHIA ASHERY
SERIKALI imesema itaweka mikakati kuhakikisha inatokomeza utapiamlo nchini na kutoa elimu ya lishe kuanzia ngazi za awali katika jamii.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, wakati akifungua warsha ya siku tatu kujadili mikakati ya kutoa elimu juu ya lishe bora.
Pallangyo alisema Tanzania inayo idadi kubwa ya watoto na wanawake wajawazito, ambao wana utampiamlo unaosababishwa na kukosekana kwa lishe bora, hali ambayo inasababisha watoto kuzaliwa na uzito mdogo, kudumaa, kuwa na upungufu wa damu, madini na vitamini.

Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania imeamua kulivalia njuga suala la lishe na kuhakikisha  inaweka mikakati mizito, ambayo itaboresha hali ya lishe kwa watoto na kutokomeza utapiamlo.
 

“Wananchi wengi hawana elimu juu ya umuhimu wa lishe bora na kama elimu itatolewa, basi kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya watoto na wajawazito wenye utapiamlo ikapungua,” alisema Pallangyo.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano, wamedumaa wakati asilimia 16 walipoteza maisha na asilimia 21 ya watoto walizaliwa wakiwa na uzito wa chini.
Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania imejiwekea mikakati ya kutomomeza utapiamlo kwa kushirikiana na wadau wengine na imekuwa nchi ya kwanza kutia saini mpango wa uanachama wa lishe bora uliotiwa saini na  Rais Jakaya Kikwete mwaka 2011.
Alisema pia Mei 2013, serikali  ilizindua kampeni ya kitaifa kwa ajili ya utekelezaji wa lishe ya kisasa, kampeni ambayo inalenga kuhakikisha jamii inazingatia ulaji wa vyakula vyenye lishe bora.
Naye mshauri wa masuala ya lishe kutoka Ujerumani, Maria Pizzini, alisema warsha hiyo itawawezesha kubadilishana mawazo na kupanga mikakati ya kutokomeza utapiamlo.
Maria alisema huu ni wakati wa kila nchi kuhakikisha inasimamia suala la lishe bora, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu.
Warsha hiyo inashirikisha washiriki kutoka nchi tisa za Afrika, ambazo ni Kenya, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Uganda, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania, pamoja na nchi mwanachama wa mpango wa lishe, ambazo ni Marekani, Uingereza, Uswisi na Bangladesh.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru