NA MWANDISHI WETU, TUKUYU
HALMASHAURI ya Wilaya Rungwe, imetenga sh. milioni 150 kwenye bajeti yake ya mwaka 2014/2015, kununua vifaa vya maabara na kufunga mifumo imara ya gesi, katika shule zake 28 za sekondari zilizoko wilayani humo.
Kiasi hicho cha fedha kitatengwa kupitia ruzuku ya kukuza mtaji katika Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alisema hayo alipokuwa akielezea mkakati wa kujenga na kutumia maabara kwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani hapa.
Veronica alisema walimu wa masomo ya sayansi waliopo ni 154, kati ya walimu 336 wanaohitajika hivyo kuna upungufu wa walimu 182 lakini kwa masomo ya sanaa hawana upungufu kwa sasa.
Alisema kimsingi, karibu shule zote 28 za sekondari zinafanya mafunzo kwa vitendo na kufanya mitihani isipokuwa mbili alizozitaja kuwa ni Kimampe na Ziwa Ngozi.
“Mkakati uliopo ni kuimarisha vyumba vinavyotumika kama maabara kwa kuhakikisha tunaziwezesha shule kutengeneza mfumo wa kusambaza gesi katika vyumba vilivyotengwa nna tayari tumefanya mazungumzo na atakayefanya kazi hiyo,” alisema Veronica.
Aliongeza kuwa sh. 500,000 zimetengwa kwa kila shule, hivyo jumla ya sh.14,000,000 zitatolewa kutoka kwenye ruzuku ya kukuza mtaji katika serikali za mitaa.
Mkurugenzi huyo alisema mikakati mingine iliyopo ni kuziwezesha shule kununua vifaa vyote vya maabara vinavyohitajika ambapo kila shule itapewa sh.milioni 1.5. alisema katika ununuzi huo sh. milioni 42 zimetengwa kupitia ruzuku ya serikali za mitaa.
Veronica aliongeza wanatengeneza stuli 994 na meza 633 zinazopungua ili kuwezesha kila mwanafunzi kuwa na meza na kiti chake anapokuwa kwenye chumba cha maabara.
“Meza na viti hivyo zitatengenezwa kutokana na miti inayoendelea kukatwa ili kutengeneza samani za shule za msingi na sekondari na sh. milioni 65 zimetengwa kwa kazi hiyo,” alisema Veronica.
Kwa mujibu wa Veronica, pia wanatarajia kumalizia ujenzi wa maabara katika shule za Isongole, Mpuguso, Lupoto na Kisiba ambapo wametenga sh. milioni 94 kwa ajili ya kazi hiyo sambamba na kuziwezesha shule za Kimampe na Lake Ngozi kununua maabara za kuhamishika ambapo kila moja itapewa sh. milioni mbili.
Mkurugenzi aliongeza wanatarajia kuanza ujenzi wa vyumba 52 ili kukamilisha idadi ya vyumba vitatu kwa kila shule ambapo kila mwaka watakuwa wanatenga kwenye bajeti kiasi cha sh. milioni 150 kwa ajili hiyo.
Kwa upande wa shule za msingi, alisema yanahitajika madawati 26,670 wakati yaliyopo ni 14,196 sawa na asilimia 53 ya mahitaji hivyo kuna upungufu wa madawati 12,474.
Kwa shule za sekondari, alisema zinahitajika meza 15,426 na viti 15,426 na kuwa zilizopo ni 14,707 na viti 14,707 hivyo kuna upungufu wa meza 719 na viti idadi hiyo hiyo.
Veronica alisema kwa sasa halmashauri inavuna msitu wake ulioko Simike ambapo mbao 6,500 zinatarajiwa kuvunwa kwa ajili ya kutengeneza madawati, viti na meza kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Alisema hadi mwishoni mwa wiki iliyopita ya mbao 2,131 zilikuwa zimepasuliwa na kuhifadhiwa ili zikauke.
Tuesday, 9 September 2014
Rungwe yapania kumaliza tatizo la mabara, madawati
07:28
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru