Tuesday, 23 September 2014

TAWOMA waomba kupatiwa mafunzo

NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Eunice Negele, amesema wanakabiliwa na changamoto  ya elimu ya uchimbaji, biashara na madini.
Hayo aliyasema jana mjini Dar es Salaam, wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho, unaofanyika kwa siku mbili kuanzia jana, uliofunguliwa na Kamishna Msaidizi wa Madini, Hamisi Komba, kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

“Lengo la chama chetu ni kuwaunganisha wanawake wachimbaji pamoja na kusaidiana kutoka mahali walipo na kuwaweka sehemu itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Lakini tunakabiliwa na changamoto ya elimu ya uchimbaji, biashara, madini na ufahamu wa thamani na ubora wake ili tufanye biashara kwa ufanisi na kuongeza kipato,” alisema Eunice.
Eunice aliishukuru serikali kwa jitihada wanazozifanya kuwapatia ruzuku ya Dola za Marekani 50,000 na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kuwapatia mikopo kwa mtu aliyetimiza masharti.
Hata hivyo, alisema wanahitaji mafunzo ya usanifu wa madini, ambayo yatawawezesha kuyatengeneza na kuyaboresha.
Awali, akifungua mkutano huo, Kamishna Msaidizi, Komba alisema serikali imekuwa ikiwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa na uongezaji thamani.
Alisema imeendelea kuwasiliana na wachimbaji hao na kutoa bei elekezi za madini mbalimbali .
Mkutano huo unatarajiwa kufungwa leo na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru