Tuesday, 9 September 2014

Wanafunzi 808,111 wa darasa la saba kufanya mitihani leo

NA RACHEL KYALA

SERIKALI imewataka wakaguzi wa elimu katika ngazi zote nchini, kuhakikisha idadi ya wanafunzi 808,111 wanaopaswa kufanya mtihani wa darasa la saba inatimia.
Aidha, imewataka wakaguzi hao kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi na walezi watakaowaelekeza wanafunzi hao kufanya vibaya katika mitihani hiyo kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa sababu zisizo za msingi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema jana kuwa, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwaagiza watoto wao kuandika madudu ili wasifaulu mtihani, badala yake kuwafanya vitega uchumi vya familia kwa kuwatafutia kazi ama kuwaozesha.
“Hivi karibuni nilifanya ziara wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma kwa lengo la kuionya jamii hiyo, ambayo imekuwa na tabia ya kuwafanyia ngoma za kuwapongeza wanafunzi wanaofeli au kutofanya mtihani wa darasa la saba na kuwataka waache tabia hiyo mara moja,” alisema.
Alisema alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha anawachukulia hatua kali za kisheria wote watakaofanya jambo hilo mwaka huu, na kuwataka wakuu wengine wa mikoa na wilaya kufanya hivyo.
Naibu Waziri huyo pia amezionya kamati za mitihani za mikoa na wilaya nchini, kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo na kuwataka wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Nawaasa wasimamizi wa mitihani kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani serikali itachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za mitihani,” alisema.
Alisema jumla ya shule 15,884 zinatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, zikiwa na jumla ya watahiniwa 808,111, wavulana wakiwa 378,470, sawa na asilimia 46.84, na wasichana 429,641, sawa na asilimia 53.16.
Alibainisha kuwa watahiniwa 783,223 watafanya mtihani huo kwa lugha ya kiswahili na 24,888 kwa kiingereza. Watahiniwa wasioona walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 86 huku wenye uoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa wakiwa 714.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru