Tuesday, 2 September 2014

Dk. Sheni ateta na marais wa Comoro na Shelisheli


Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Sheni, amekutana na kufanya mazungumzo na marais James Michel wa Shelisheli na Ikililou Dhoinine wa Comoro, ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo.

Mazungumzo kati ya Dk. Sheni na marais hao, yalifanyika juzi sambamba na Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa, unaoendelea mjini Apia katika visiwa vya Samoa, ambako marais hao wanahudhuria.
Katika mazungumzo yake na Rais wa Shelisheli, Dk. Sheni alimhakikishia kuwa Tanzania inaunga mkono Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabiachi (Western Indian Ocean Coastal Challenges-WIO-CC), ambao unatarajiwa kuzinduliwa leo mjini Apia.
Viongozi hao walikubaliana kuwa mpango huo ni muhimu kwa kuwa unatoa fursa ya kuziweka nchi hizo karibu katika kushughulikia changamoto zinazozikabili ambazo wakati mwingine hazipewi nafasi zinazostahili katika majukwaa ya kimataifa. Mpango huo unashirikisha visiwa vya Comoro, Madagascar, Reunion, Shelisheli na Zanzibar.
Dk. Sheni na Rais Michel walieleza dhamira za serikali na wananchi wa nchi zao kuimarisha ushirikiano kwa kuangalia maeneo mengi zaidi, ambayo nchi hizo zinaweza kushirikiana na kuwa na manufaa kwa nchi zote.
Akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Comoro, Dk. Sheni alimueleza kuwa amefurahi kuona maandalizi ya mpango wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Comoro yanaendelea vyema, ambapo maeneo ya ushirikiano yameainishwa na yanafanyiwa kazi.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni afya, elimu, utamaduni, miundombinu na kilimo, ambapo Zanzibar na Comoro zinaweza kushirikiana katika utafiti wa mazao ya kilimo .
Dk. Sheni alimhakikishia Dhoinine kuwa Zanzibar iko tayari kuisaidia nchi yake kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuwapatia fursa za masomo ya shahada za uzamili na uzamivu katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Sambamba na hatua hiyo, alimueleza Rais huyo kuwa Zanzibar inaweza kuwapatia mafunzo ya lugha hiyo waandishi wa habari na watengeneza vipindi vya redio na televisheni wa Comoro ili kukuza uwezo wao wa kutengeneza vipindi kwa lugha ya Kiswahili.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Comoro, Ikililou Dhoinine alimueleza Dk. Sheni kuwa ingawa wananchi wengi wa nchi yake wanasikia na kufahamu vyema lugha ya Kiswahili, lakini wengi hawawezi kukizungumza kwa ufasaha.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwa televisheni na redio za nchi hiyo zinatangaza vipindi kwa lugha ya Kiswahili, vipindi hivyo ni vichache kutokana na watangazaji wachache wanaozungumza lugha hiyo.
Dk. Sheni yupo nchini Samoa kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaoendelea hapa kwa siku nne.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru