Thursday 11 September 2014

Jaji Mutungi atangaza vita


  • Wanachama vyama vyote nchini kuhakikiwa
  •  Teknolojia mpya kutumika kubaini ubabaishaji
NA RABIA BAKARI
UBABAISHAJI na uendeshaji wa ujanja ujanja wa baadhi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumua nchini, umeanza kuitisha Ofisi ya Msajili na sasa inajiandaa kuvifanyia uhakiki ili kubaini udanganyifu.
Hatua hiyo inalenga kufichuliwa kwa vyama vyote vinavyoendeshwa kwa ujanja ujanja ama kutokuwa na vigezo vya kuendelea kuwa na usajili wa kudumu kutokana na mabadiliko mbalimbali.
Habari za kuaminika zimebainisha kuwa, kuna baadhi ya vyama vina usajili wa kudumu, lakini kwa sasa havina vigezo kutokana na kuzorota kwa uendeshaji wake na vingine kukimbiwa na wanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alisema baada ya uhakiki huo, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Alikuwa akipokea msaada wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP).
Alisema mwanzo ilikuwa ngumu kufanya uhakiki ama kuwa na majibu ya haraka, hivyo baadhi ya vyama kupata mwanya wa kufanya udanganyifu.
“Tumepokea vitendea kazi vyote kuanzia kompyuta za mezani, skana, simu za mkononi na kompyuta mpakato. Kusema kweli hatuna cha kusingizia isipokuwa kuwahakikishia Watanzania matokeo mazuri katika utendaji kazi wetu.
“Sasa hakuna chama kitakachodanganya, kikisema Mtwara kina wanachama kiasi kadhaa au kuna hili na lile, tunaingia mtandaoni na kuthibitisha,” aliongeza.
Alisema kadri wanavyoboresha ofisi hiyo, ndivyo atakavyojitahidi kuboresha vyama ili mawasiliano yaende sambamba na kuhakikisha hakuna atakayeachwa nyuma.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Phillipe Poinsot, alisema vifaa hivyo vina thamani ya sh. milioni 400, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha demokrasia nchini (DEP), ulioanza kutekelezwa na Ofisi ya Msajili mwaka huu.
Alisema mradi huo upo kwa takriban vipindi viwili vya uchaguzi, lakini ukiwa unatekelezwa na ofisi tofauti, ikiwemo Tume ya Uchaguzi Bara (NEC) na Zanzibar (ZEC), kabla ya kuhamishiwa katika ofisi hiyo.
Meneja Mtekelezaji wa DEP, Beatrice Stephano, alisema tayari wamepokea sh. milioni 500 za kuanza utekelezaji wa mradi, ambapo ukomo wake utategemea ufanisi wa utendaji katika mradi huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru