Tuesday 2 September 2014

Wananchi Kilombero wamfagilia JK


Na Igamba Libonge, Kilombero
RAIS Jakaya Kikwete ameelezwa kuwa ni kiongozi aliyejitosa kikamilifu kuwakomboa Watanzania kiuchumi na kuwafanya hivi sasa watembee kifua mbele.
Kauli hiyo imetolewa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutoka wilaya ya Kilombero, Kanali Mstaafu, Haruni Kondo wakati wa sherehe maalumu ya kumpongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara wilayani Kilombero.
Ziara hiyo imeleta matumaini makubwa kwa wakazi wa Kilombero, hasa utimizaji wa ahadi za Rais Kikwete tangu alipoingia madarakani. Sherehe hizo zilifanyika katika kata ya Mwaya, tarafa ya Mang˙la wilayani humo.
Kanali Kondo alisema tangu Rais Kikwete alipochukua hatamu za uongozi wa nchi mwaka 2005, amefanya maendeleo na mapinduzi katika nyanja zote za uchumi, siasa na kijamii na amepanua na kuboresha sekta ya elimu, afya, miundombinu, maji, umeme na mawasiliano na Watanzania wote ni mashuhuda wa mafanikio hayo.
Alisema wananchi wa Kilombero wameona wafanye sherehe kubwa ya kumpongeza kwani watakuwa wachoyo wa fadhila kama hawataonyesha shukrani zao za dhati kwa kumpa nguvu kiongozi wao katika juhudi zake kubwa za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka tisa sasa cha uongozi wake, Rais Kikwete na serikali ya CCM,
wameweza kujenga kilometa 11,000 za barabara kwa kiwango cha lami, daraja la Kigamboni linaloendelea kujengwa, kivuko cha mto Malagalasi na ujenzi wa daraja la mto Kilombero.
Alisema pia kuwa utawala wa Rais Kikwete umeweza kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kutumia rasilimali na uwezo wa nchi, badala ya kuomba na kutegemea misaada ya nje, sambamba na kupanua sekta ya elimu, hususan sekondari kwa kuanzisha shule za kata hivyo kuwezesha huduma hiyo muhimu karibu na wananchi.
Alisema wananchi wa wilaya ya Kilombero wanampongeza na kumshukuru kwa kutekeleza ahadi alizozitoa, ikiwemo ujenzi wa daraja katika mto Kilombero na mchakato wa ujenzi wa barabara kutoka Mikumi hadi Ifakara na barabara ya kutoka Ifakara kwenda Mlimba kwa kiwango cha lami.
Aidha, amempongeza Rais Kikwete kwa maamuzi ya kijasiri aliyoyachukua ya kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa ghala la chakula na pia mpango alioutangaza hivi karibuni katika ziara yake wilayani hapa wa kupanua na kuendeleza zao la miwa katika bonde la Kilombero kwa kujenga viwanda 10 vya sukari.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru