NA EVA-SWEET MUSIBA, BUNDA.
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amepunguza bei ya kivuko cha MV Mara kutoka sh. 2,000 hadi sh. 500 kwa mtu mmoja.
Magufuli pia ameamuru kivuko hicho kisiwatoze nauli wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapokuwa wamevaa sare za shule.
Waziri huyo wa ujenzi alitoa agizo hilo jana baada ya kukizindua kivuko kipya cha MV Mara, kitakachoanza kufanya safari zake kutoka kijiji cha Mugala-Kwiramba wilaya ya Bunda kwenda Majita-Kurugee wilayani Butiama.
Kivuko hicho chenye uzito wa tani 25 na chenye uwezo wa kubeba abiria 50, kimeigharimu serikali sh. milioni 545.2.
Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kivuko hicho, Magufuli alisema kitaokoa maisha ya wananchi wengi, ambao walikuwa wakipata adha kubwa ya usafiri katika maeneo hayo kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika.
Magufuli alisema kivuko hicho kitakuwa kikitoza nauli ya sh. 500 kwa watu wazima wakati wanafunzi waliovaa sare, hawatatozwa nauli. Awali, wananchi walikuwa wakilipa nauli sh. 2,000.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kwiramba walisema, walikuwa wakipata tabu kubwa ya usafiri na kulazimika kutumia mitumbwi na hivyo kuhatarisha maisha yao.
Mbali na kuzindua kivuko hicho, Magufuli pia alikagua mradi wa barabara ya Bunda-Mwibara, ambayo itajegwa kwa kiwango cha lami na kugharimu sh. bilioni 52.2.
Tuesday, 8 July 2014
Magufuli ni kiboko
01:55
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru