Wednesday 2 July 2014

Basi la mahabusu lashambuliwa Dar



  • Lamiminiwa risasi mfululizo, watatu wajeruhiwa 
  • Balozi wa Libya nchini ajiua kwa risasi ofisini

NA MWANDISHI WETU
GARI la Magereza lililokuwa limebeba mahabusu likitokea Mahakama ya Mwanzo Kawe kwenda Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, limeshambuliwa kwa risasi na mtu asiyefahamika.

Wakati tukio hilo likitokea jana mchana maeneo ya Mikocheni na kusababisha askari Magereza wawili, akiwemo dereva na mahabusu kujeruhiwa,
aliyekuwa Kaimu Balozi wa Libya, Ismail Nwairat, alifariki dunia kwa kujipiga risasi.
Kamanda wa Polisi, mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha jana kutokea kwa tukio la gari la mahabusu kushambuliwa kwa risasi, alipozungumza na Uhuru kwa njia ya simu.
“Ni kweli kwamba mtu asiyefahamika leo (jana), saa saba mchana, maeneo ya Mikocheni, alilishambulia kwa risasi gari la kubeba mahabusu lenye namba MT OO46 lililokuwa likitokea Mahakama ya Kawe kwenda Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na baadae Segerea,” alisema.
Kamanda Wambura alisema gari hilo, lilipofika maeneo ya Mikocheni, mtu asiyefahamika alilirushia risasi na kusababisha kuvunja vioo vya upande wa kulia na nyuma vya gari hilo na kusababisha majeraha kwa watu watatu.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Sajeni Msofe, aliyepata michubuko katika kiganja chake cha mkono wa kulia, Koplo Dotto ambaye alijeruhiwa kwenye matiti na mahabusu Dorine Damian ambaye alipata mchubuko katika paji la uso na bega la kulia.
Kamanda Wambura alisema katika tukio hilo, hakuna mahabusu aliyetoroka wala kutoroshwa kwa kuwa askari Magereza walikuwa imara na kuimarisha ulinzi.
Alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini mtuhumiwa huyo ambaye alitoweka ni nani na alikuwa na madhumuni gani ya kufanya kitendo hicho.
Kuhusu tukio la kujipiga risasi Kaimu Balozi wa Libya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema Nwairat alijipiga risasi juzi saa saba mchana, ofisini kwake katika jengo la Ubalozi wa Libya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Wizara hiyo, Nwairat alijifungia ofisini na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto. 
Ilisema kuwa maofisa wa ubalozi waliposikia mlipuko wa bunduki, walivunja mlango na kumkuta Kaimu Balozi huyo ameanguka chini. 
Taarifa hiyo ilisema Nwairat alipelekwa katika Hospitali ya AMI, Oysterbay ambako ilielezwa kwamba alikwishafariki.  
Ilisema maiti ilihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). 
Taarifa hiyo ilisema Ubalozi unafanya maandalizi ya kusafirisha mwili wa Nwairat kwenda nyumbani kwao kwa mazishi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuhakikishia Ubalozi wa Libya ushirikiano wake katika kipindi hiki kigumu. 
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa za awali walizonazo ni kwamba alijipiga risasi.
Advera alisema wanasubiri taratibu za kidiplomasia zikamilike ili waweze kuendelea na uchunguzi kuhusu kifo hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru