NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA
BARAZA la Madiwani wa Jiji la Mbeya limeridhia kusamehe deni la zaidi ya sh. bilioni 1.3 kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Chuo hicho kilikuwa kinadaiwa kiasi hicho kutokana na kuuziwa kiwanja namba 8 kilichoko katika kitalu G eneo la Iwambi, ambapo kilikuwa kimelipa sh.1,070,000,000 kati ya sh. 2, 417,700,000 kilizokuwa kinadaiwa na jiji hilo.
Hayo yalifikiwa juzi, ambapo wajumbe wote walikubali kusamehe deni hilo ili uwe mchango wa halmashauri katika kusaidia kuinua sekta ya elimu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madiwani walisema awali walikuwa hawaelewi vizuri kuhusu deni hilo, lakini kwa kuwa ufafanuzi mzuri ulitolewa na Kamati ya Fedha na Utawala, shaka waliyokuwa nayo imeondoka.
Diwani wa Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki, alisema awali alikuwa miongoni mwa madiwani waliokuwa wakipiga kelele kuhusu kiasi hicho cha fedha kutolipwa na hilo lilichangiwa kutoelezwa kwa kina kama ilivyofanyika kwenye kikao hicho.
Aliongeza kuwa, katika kata yake kuna Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) ambacho kimeifanya kuwa na maendeleo makubwa tofauti na awali ambapo ilionekana kama iko porini.
Naye Meya Athanas Kapunga, aliwashukuru wajumbe wa baraza hilo kukubali kusamehe deni hilo ili nao waingie kwenye historia kuwa katika kipindi chao cha uongozi waliwezesha chuo hicho kujengwa.
“Awali niliambiwa sifai kutokana na suala hili la kiwanja hiki, lakini leo nawashukuru madiwani wenzangu kutambua umuhimu wa Mzumbe kusamehewa deni hili ili nasi katika uongozi wetu tuingie kwenye historia kuwa tulitoa mchango wetu kwa Chuo Kikuu hiki,” alisema Kapunga.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe chini ya Mkuu wake, Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samata na ule wa jiji chini ya Meya Kapunga ulikutana Julai 4, mwaka huu, kujadili namna ya chuo kitakavyomaliza deni lililobaki, ambapo kiliwasilisha ombila kusamegewa kutokana na kutopata fedha ya miradi ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo.
Saturday, 12 July 2014
Mzumbe yasamehewa mamilioni
09:21
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru