Wednesday 2 July 2014

UKAWA kitanzini na mwandishi wetu


VIONGOZI na wanasiasa wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wametakiwa kutumia busara na kuyafanyiakazi maagizo ya viongozi wa dini ya kuwataka kurejea bungeni.
Pia wametakiwa wajitafakari wenyewe na kwamba hawastahili kubembelezwa wala kulazimishwa kuhusiana na kurejea bungeni kwani, wananchi ndio waliowatuma kufanyakazi hiyo na si vinginevyo.
Kauli hizo zilitolewa jana na wasomi na wanasiasa walipozungumza na gazeti hili kuhusu kauli iliyotolewa juzi na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Severine Niwemugizi, wakati akitoa salamu za baraza hilo katika Jubilei ya kutimiza miaka 25 ya Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Iringa, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa.
Baraza hilo liliitaka serikali kuhakikisha wajumbe wa UKAWA wanarejea bungeni bila masharti kwani, Bunge Maalumu la Katiba lipo kisheria na kitendo cha wajumbe hao kususa ni kuwasaliti Watanzania.
Limewataka wabunge hao kurejea kwenye bunge hilo linalotarajiwa kuendelea mwezi ujao kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya na kwamba, hilo ni agizo wala si ombi.
Hata hivyo, limeonya kuwa iwapo wataendelea kukaidi, wananchi wasiwachague tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwani, watakuwa wameshindwa kuonyesha uwajibikaji.
Dk. Benson Bana, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema mawazo yaliyotolewa na TEC ni dhahiri kwa sababu UKAWA hawakutoka bungeni kwa kufuata sheria hivyo, wasibembelezwe.
Alisema viongozi hao wanatakiwa watafakari Watanzania wanatarajia nini kutoka katiba Bunge la Katiba na sababu za  wajumbe hao kuwemo.
“Hata wakipima safari zao za mikoani na mamilioni waliyotumia na kutathmini zimezaa matunda gani na ikiwezekana watafute taasisi iwafanyie utafiti ili kujua ziara zao kama zimefanikiwa,” alisema.
Alisema busara yao iwatume warejee na kuzungumza masuala yao kwa kutumia kanuni, miongo na taratibu kwani, kutoka nje hakusaidii.
Dk. Bana alisema mkakati waliotumia wa kutoka nje si sahihi kwani wananchi wanatarajia kupata katiba na si malumbano na hawawezi kufanikisha jambo lolote linalohusu bunge hilo wakiwa nje.
Alisema licha ya kuwa na hoja za msingi ni lazima warudi na kwenda kuzizungumza ndani ya bunge na ikiwezekana waombe kuonana na Rais Jakaya Kikwete na kuwasilisha malalamiko yao na si kuzunguka mikoani.
Naye Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP),alisema  UKAWA hawana haki ya kususia bunge hilo kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kuwasaliti wananchi wanaowawakilisha.
Alisema hata kama walikuwa na matatizo, hawakupaswa kutoka nje bali walitakiwa kutumia kamati ya maridhiano, ambayo waliikwepa na kwenda kwa wananchi jambo ambalo ni kinyume na demokrasia.
Mrema alishauri UKAWA warejee bungeni bila ya masharti kama walivyoingia ili taifa liweze kufanikisha malengo ya uundwaji wa katiba mpya kama ilivyokusudiwa.
Aidha, alisema UKAWA ni lazima watambue kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu uundwaji wa katiba mpya si ya wabunge bali yatatolewa na wananchi.
“Sielewi kwa nini UKAWA wanataka kupoka madaraka ya wananchi ambayo yapo kisheria, waache kuhamasisha vurugu, warudi bungeni,” alisisitiza Mrema.
Pia, aliwataka waliokuwa viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukaa kimya kwa kuwa muda wao wa kazi ulishamalizika.
Naye, Waziri Mkuu Pinda alisema serikali imepokea wito wa Baraza hilo la kuwataka UKAWA warejee bungeni, mara bunge hilo litakapoanza ili Katiba itakayojadiliwa iwe kwa maslahi ya watanzania wote na sio wachache.
Aliwataka UKAWA kurudi ili wakabishane ndani ya bunge na kufikia muafaka huku wakitafakari nchi ilikotoka, ikiwa na serikali mbili zilizo ndani ya taifa moja.
Kumekuwepo na madai mbalimbali kuhusiana na sababu za UKAWA kususia vikao vya bunge hilo, baadhi wakidai kuwa wamekuwa wakilipwa na taasisi fulani za kimataifa kwa lengo la kukwamisha mchakato huo.
Madai hayo yamekuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wanasiasa na hayajawahi kupatiwa majibu wala kutolewa ufafanuzi hivyo, kuzusha sintofahamu. 
Viongozi wa UKAWA jana hawakuweza kupatikana kuzungumzia agizo hilo la viongozi wa dini, ambapo baadhi simu zao za kiganjani zilikuwa zikiita bila majibu na zingine kuzimwa kabisa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru