NA ANTAR SANGALI, ZANZIBAR
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakina ubia wa sera na CUF katika uendeshaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Sheni.
Msimamo huo wa CCM, imetokana na kauli ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, kudai hivyo, wakati akihojiwa na kituo kimoja cha luninga, hivi karibuni.
Msimamo huo ulitolewa jana na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Itikadi na Uenezi (Zanzibar), Waride Bakari Jabu, wakati akizungumza na viongozi wa matawi, mashina, wadi na jimbo katika Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema CCM imeshitushwa na upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na Maalim Seif, kwa kueleza kuwa Dk. Sheni huchukua baadhi ya sera za CUF akichanganya na za CCM katika uendeshaji wa serikali.
Waride alisema Maalim alikusudia kupotosha umma kwa maslahi yake kisiasa na kwamba, kauli hiyo inapaswa kupuuzwa kwani haina ukweli.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Chama kinachoshika nafasi ya urais ndiyo huendesha serikali na mawaziri wote hutakiwa kusimamia na kutekeleza bila ya ubia au ushirika wa kisera na chama.
“CCM inamtaka Maalim Seif kuaacha upotoshaji wake, CCM haina ubia wala ushirika na CUF wa kisera na jambo hilo halitazamiwi kutokea. Ilani ya CCM ya mwaka 2010/2015 ndiyo inayosimamia uendeshaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema Waride.
Aidha, alimtaka Maalim Seif kuacha chokochoko za kisiasa na kwamba, matamshi yake yanalenga kumgonganisha Dk. Sheni na CCM.
“Tunamtambua Maalim Seif ni mwanasiasa anayependa siasa za uchonganishi na fitina, anachokifanya ni kuanza chokochoko mpya kwa lengo la kukiyumbisha Chama chetu na kuwavuruga wana-CCM.”
“Hatuna ubia wala ushirika wa kisera na CUF,” alisema Waride, ambaye ni Mwakilishi wa Kiembesamaki.
Thursday, 17 July 2014
CCM Zanzibar yamshukia Maalim Seif
07:54
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru