Monday, 21 July 2014

Waomba upelelezi uharakishwe


NA FURAHA OMARY
UPANDE wa utetezi katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime na wenzake 10, umeomba upande wa jamhuri ukamilishe upelelezi, ili waendelee na hatua nyingine.
Ombi hilo lilitolewa jana na wakili wa upande huo, John Mhozya, mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, wakati shauri hilo lilipokuwa linatajwa.
Mhozya aliwasilisha ombi hilo muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, kudai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
“Tunaomba upande wa jamhuri utueleze hatua ya upelelezi ulipofikia kwa kuwa umechukua muda mrefu. Tunaiomba mahakama itoe amri kwa upande huo wakamilishe upelelezi, ili tuendelee na hatua nyingine,” aliomba Mhozya.
Wakili Kongola alidai hawatakiwi na mtu yeyote kusema kuhusu hatua ya upelelezi na kuomba kuelezwa iwapo kuna kifungu cha sheria ambacho kinawataka wafanye hivyo.
Akijibu hoja hiyo, Mhozya alidai licha ya upande wa jamhuri kutatakiwa kuripoti juu ya hatua ya upelelezi ilipofikia,  unatakiwa kukamilishwa kwa muda muafaka.
Mhozya alidai shauri hilo lipo mahakamani kwa takriban miaka miwili sasa, hivyo iwapo upande wa jamhuri hautaamriwa kuhusu upelelez,i linaweza kuchukua miaka 10.
Hakimu Devotha alisema mahakama haiwezi kusema lolote kuhusu upelelezi, kwa kuwa jalada halisi la kesi hiyo lipo Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 4, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya watu 27 yanayodaiwa kutokea Machi 27, mwaka jana, baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 katika mtaa wa Indira Gandhi ni mmiliki wa jengo hilo, Raza Ladha.
Pia wamo Mhandisi wa jengo hilo, Goodluck Mmbanga, mkaguzi wa jengo Willbrod Mugyabuso, Diwani wa Kata ya Goba, Ibrahim Kissoky ambaye ni mfanyabiashara  anayemiliki kampuni ya Lucky  Construction ya Dar es Salaam,  iliyojenga jengo hilo.
Wengine ni Mhandisi Mohamed Abdulkarim, Mhandisi wa manispaa ya Ilala Charles Ogare, Mhandisi Mshauri Zonazea Oushoudada (60) anayemiliki kampuni ya Sou Consultancy Co. Ltd, ambayo ilikuwa ikisimamia ujenzi wa jengo hilo, Msanifu Majengo Vedasto Nzikoruhale (59) na mwandaaji michoro ya majengo,  Michael Hema (59).
Wengine ni Msajili Msaidizi wa Bodi ya Wasanifu na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Albert Mnuo  na Ofisa Mtekelezaji Mkuu wa AQRB, Joseph Ringo .

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru