Tuesday, 8 July 2014

RC alilia makao makuu yahamie Dodoma


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA.
WAUMINI  na viongozi wa dini mkoani hapa, wameombwa kuomba dua maalum ili azma ya  serikali ya kuhamishia makao makuu  Dodoma itimie.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi, alipokuwa akitoa salamu za mkoa kwenye mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa wanawake (UWT).
Mkuu huyo wa mkoa alisema ni vyema sasa kukawa na dua maalumu la kuombea uhamisho wa makao makuu kuwa Dodoma, kwani umekuwa wa muda mrefu sasa.
Alisema azma hiyo ya serikali ni ya siku nyingi, hivyo ni muhimu sasa ikatimizwa na kuhakikisha serikali inahamia mkoani Dodoma.
“Wakina mama nawaomba mtuombee dua ili  serikali  itimize ahadi yake,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Dodoma ina miundombinu ya kutosha kuwa makao makuu ya nchi hivyo hakuna sababu ya kutohamia.  
Aidha Mkuu huyo aliwataka wakina mama nchini kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi  wa serikali na mtaa na uchaguzi mkuu.
Aliwataka wanawake wasijione  wanyonge, kwani wana nafasi kubwa katika uchaguzi huo na wasisite kugombea.
 “Viongozi au wale waliopata uongozi kupitia UWT ni vyema wakafanya kazi zao vizuri huku wakikumbuka kuwa nafasi hizo ni za wanawake na hivyo wawatumikie wenzao kwa moyo wao wote,’’ alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru