Thursday, 3 July 2014

Daktari atuhumiwa kuiba dawa Igunga


Na Abdallah Amiri, Igunga
MKUU wa wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, Elibariki Kingu, ameiagiza polisi wilayani kwake, kumkamata mganga aliyeuza dawa katika zahanati iliyoko kata ya Sungwizi, wilayani Igunga.
Kingu alitoa agizo hilo jana,  alipotembelea kata ya Sungwizi, katika ziara za kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Alisema alishangazwa na taarifa za wananchi kuwa zahanati katika kata ya Sungwizi haina dawa kutokana na kuibwa zote, pasipo kutolewa taarifa sehemu yoyote.
Baada ya  kupata taarifa hiyo, mkuu wa wilaya  alimtaka mganga wa zahanati hiyo, John Malaba kutoa maelezo kuhusiana na wizi huo.
Hata hivyo mganga huyo alikimbia muda mfupi baada ya mkuu wa wilaya kufika.
Polisi wa eneo hilo walipoulizwa, walidai kuwa hawana taarifa yoyote juu ya jambo hilo.
Kutokana na maelezo ya polisi kwa mkuu wa wilaya, Kingu alitoa maagizo ya kusakwa kwa mganga huyo na kuwahakikishia  wananchi kwamba, hataondoka mpaka Mabala apatikane na kuwekwa kitimoto mbele ya wananchi.
Kingu alilazimika kutoa sh. 50,000 kwa polisi ili  wajaze mafuta gari lao na kumsaka  mganga huyo. Hata hivyo, hawakufanikiwa kumtia mbaroni, ambapo taarifa zinasema alikimbilia Nzega.
Mganga huyo pia anatuhumiwa kuwachangisha wananchi michango ya sh. 10,000 kwa ajili ya kujiunga na CHF bila kuwapatia stakabadhi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru