Saturday, 12 July 2014

Muarobaini ulipuaji wa mabomu watimia


Na Rabia Bakari
SERIKALI imesema imeweka mikakati ya kudhibiti milipuko ya mabomu inayoendelea kutokea nchini.
Akizungumza na Mzalendo, juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema hawezi kutaja aina ya  mikakati, lakini ipo na ni mikubwa.
“Tumejipanga kikamilifu na kwa nguvu zote kukomesha hali hii, tukisema tutafanya nini itakuwa si vizuri maana tutawapa maadui zetu nafasi ya kutujua, lakini wewe fahamu mikakati ipo na mikubwa,” aliongeza.
Aliwataka wananchi kuwa wepesi wa kutoa taarifa pale wanapohisi kitu au mtu mbaya na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzie.
Alisema licha ya vyombo vya usalama kuwepo, lakini mlinzi wa kwanza ni mwananchi mwenyewe.
Waziri Chikawe aliongeza kuwa nguvu iliyowekwa kudhibiti uhalifu wa namna hiyo na kuwepo kwa ushirikiano wa wananchi, kutasaidia kukomesha hali hiyo haraka.
Matukio ya ulipuaji mabomu yameonekana kufanyika mara kwa mara, huku maeneo yanayohusika yakiwa yale yenye rasilimali za utalii ambapo chanzo chake hakijulikani.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema hali ya usalama nchini iko ‘tambarare’ingawa kuna matukio machache yanachafua sifa hiyo, ikiwemo milipuko ya mabomu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu,  alipotembelewa na Mwenyekiti wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO), Luteni Generali Sebastian Ndeitunga ofisini kwake, Dar es Salaam.
Alisema Tanzania ni mojawapo ya nchi inayotoa kipaumbele katika suala la usalama na kwamba, kwa sasa wananchi wanashirikishwa kikamilifu kulinda amani na usalama wao.
Aliwataka watu kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa ili kuweza kuwabaini wahalifu ambao hawana nia njema na taifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru