Thursday, 10 July 2014

Dk. Sheni aweka msimamo bei ya karafuu


NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutekeleza uamuzi wake wa kuwapatia wakulima bei ya karafuu ya asilimia 80 ya bei ya soko la nje.
Dk. Sheni alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wakulima wa zao hilo wakati akizindua rasmi msimu wa ununuzi wa karafuu wa mwaka 2014/2015 uliofanyika katika ukumbi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar  (ZSTC), wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.


Alibainisha kuwa huo ni uamuzi wa kisera na kwamba Serikali haitarudi nyuma kwa kuwa lengo lake ni kihakikisha karafuu inaendelea kuwa zao la biashara kwa Zanzibar.
Alifafanua kuwa kuwapatia wakulima bei hiyo ni miongoni mwa hatua nyingi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba kuhakikisha karafuu za Zanzibar zinaendelea kuwa na ubora wake na kubaki kuwa utambulisho wa visiwa hivyo. 
Dk. Sheni alizitaja hatua zingine kuwa ni pamoja na kuimarisha huduma za ununuzi wa karafuu, kujenga barabara kwenye maeneo yenye karafuu nyingi, kutoa miche ya mikarafuu kwa wakulima, kutafuta masoko ya nje na kuwatia mikopo wakulima.
Hatua nyingine, aliongeza kuwa ni kufanya uamuzi wa kuifanyia marekebisho makubwa ZSTC ili iweze kutekeleza majukumu yake kulingana na mazingira ya sasa.
Dk. Sheni alieleza kutoridhidhwa kwake na hatua ya baadhi ya wakulima kutorejesha mikopo kwa shirika hivyo alitoa wito  kuirejesha kwa kuwa  serikali haipendi kuwapeleka katika vyombo vya sheria.
Alihimiza jitihada zaidi kwa wakulima wa karafuu pamoja na wananchi kwa jumla kutilia mkazo ulinzi katika mashamba yao ili kudhibiti wizi. Alikemea vitendo vya wezi wa karafuu hukata matawi ya mikarafuu wakati wakifanya vitendo hivyo viovu.
Kabla ya uzinduzi huo, Dk. Sheni alitembelea mashamba ya karafuu katika kijiji cha Tumbi –Chumbageni katika Wilaya ya Chakechake na kuona namna mkulima Said Sinani alivyoimarisha shamba lake la miaka mingi na shamba jipya la mikarafuu la wakulima Mbarouk Abdalla Mohamed na Songoro Shaaban Songoro.
Alitangaza bei hizo kuwa ni karafuu daraja la kwanza itakuwa ni 14,000 kwa kilo, daraja la pili 12,000 kwa kilo na daraja la tatu 10,000 kwa kilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru