Monday 21 July 2014

Wachimbaji wafa mgodini Mirerani


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WACHIMBAJI wadogo wawili katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, wamekufa na wengine watatu kujeruhiwa, baada ya kulipuliwa na baruti wakiwa mgodini. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 7:30 mchana, eneo la Kitalu B, Mirerani, katika mgodi unaomilikiwa na Mike Oscar (34), mkazi wa Sanya Juu, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.
Imeelezwa kuwa baruti hiyo ilipigwa kutoka katika mgodi unaomilikiwa na Valerian Palangyo na  kuwajeruhi wafanyakazi wa mgodi wa jirani.
Kwa mujibu wa polisi,  baruti ililipuliwa chini mgodini na kusababisha vifo vya watu hao waliokuwa kwenye mgodi wa jirani.
“Wachimbaji wa migodi hiyo miwili walikuwa wanaendelea na kazi, baruti ilipigwa kwenye mgodi wa Pallangyo na kutoboa chini kwenda katika mgodi wa pili,” alisema  Nsimeki.
Aliwataja waliokufa kwenye tukio hilo kuwa ni Bernard Fredrick (28) na Kuii Habi (32),  wakazi wa Mirerani. Miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru.
Waliojeruhiwa kwenye tukio hilo ni Adam Juma (29), Hussein Emili (32) na Isaya Reuben (32) .
Alisema majeruhi  wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo  na hali zao zinaendelea vizuri.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru