Saturday, 12 July 2014

Dk. Migiro: Chukueni hatua za matukio hatari


NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, amezitaka idara zinazohusika na jukwaa la haki jinai kuchukua tahadhari dhidi ya matukio yanayohatarisha usalama wa taifa.
Migiro alisema hayo jana katika ufunguzi wa kikao cha mawaziri na watendaji wa taasisi zinazounda jukwaa la haki jinai.
Alisema katika kukabiliana na matukio hayo, ushirikiano wa pamoja unahitajika katika utendaji kazi ili kudhibiti hali hiyo.
Dk. Migiro alisema mwenendo wa matukio ya uhalifu unaweza kukabiliwa kwa kuchukua tahadhari ushirikiana na vyombo  mbalimbali vya usalama.
“Ni lazima tushirikiane kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na taifa kwa ujumla,” alisema
Alisema yapo matukio yanayohatarisha usalama ambayo yanaweza kutokea katika nchi jirani ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa taifa ambayo yanatakiwa kuchukuliwa tahadhari mapema.
“Mhalifu hana rangi wala kabila wala taifa, ni lazima kuhakisha tunatambua vitu kama hivyo na kuchukua tahadhari,” alisema.
Pia alisema yapo matukio ya uhujumu wa maliasili za nchi kama wanyamapori na nyinginezo, suala ambalo linatakiwa kila mmoja anayehusika na idara hiyo kusimamia kuhakikisha hayatokei.
Alisema jukwaa hilo ndilo lenye dhamana ya kudhibiti masuala yanayohusu jinai sambamba na kuhakikisha wanasimamia haki za watoto, walemavu na wanawake.
“Japokuwa kuna maneno yanayosemwa, watoto wanaozaliwa katika ndoa sio halali, lakini ni lazima tuzingatie kwa ufasaha suala vinasaba,” alisema
Alisema lipo suala la wanaume kuruka majukumu yao na kusisitiza kuwepo kwa haja ya kuzingatia vinasaba ili kuweza kukabilina na suala hilo.
Kwa upande wake, Hassan Nkussa ambaye ni msimamizi wa upelelezi na uendeshaji wa mashitaka katika Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema iwapo matukio ya milipuko ya mabomu, tindikali na ujangili havitadhibitiwa, yanaweza kuathiri sekta ya utalii na kushusha pato la taifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru