Wednesday, 9 July 2014

Bomu latikisa Arusha  •  Lalipuka mgahawani, wanane wajeruhiwa
  •  Watuhumiwa wawili mbaroni, 25 wasakwa
  •  Kamati ya usalama ya mkoa yalaumiwa

WAANDISHI WETU, ARUSHA NA DAR
WATU wanane wakiwemo wanne wa familia moja  wenye asili ya kiasia, wamelipukiwa na bomu na kujeruhiwa vibaya wakati wakila chakula cha jioni katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cusine uliopo mtaa wa Uzungunni mjini Arusha.
Tukio hilo ambalo ni la sita kutokea jijini Arusha, lilitokea juzi, saa 4.30 usiku, katika mgawaha huo uliopo jirani na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha.
Matukio mengine ya bomu kutokea Arusha ni pamoja na lile lililotokea katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa CHADEMA, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Olasiti na juzi la Sheikh kulipuliwa bomu nyumbani kwake.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku nne, baada ya Mkurugenzi  wa Taasisi ya Kiislamu ya Answar Muslimu Youth Centre, Kanda ya Kaskazini,  Sheikh Sudi Ally Sudi na mgeni wake, Muhaji Kifea kulipuliwa na bomu nyumbani kwa Sheikh huyo eneo la Majengo, Arusha wakati wakila daku.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Kamishna Isaya Mngulu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari polisi inawashilia watu wawili kwa mahojiano.
KAIMU MGANGA MKUU AZUNGUMZA
Kaimu  Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani ya Seliani, Dk. Poul Kisanga, amesema miongoni mwa majeruhi hao, Deepak Gupta (25), yuko katika hali mbaya na amehamishiwa  katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), baada ya kupoteza mguu wa kushoto kufuatia mlipuko huo.
Alisema majeruhi hao walifikishwa hospitalini hapo saa 5.00, usiku, na watano kati yao walikuwa na hali mbaya na walipelekwa moja kwa moja katika chumba cha upasuaji na kwamba upasuaji ulifanyika mpaka alfajiri ya jana.
Dk. Kisanga alisema katika majeruhi hao, wapo watu wanne wa familia moja, akiwemo baba, mama na watoto wawili.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Manci Gupta (14), mama yao Manisha Gupta (36), baba yao Mahush  Gupta (42) na Deepak ambaye amepoteza mguu wa kushoto.
Dk. Kisanga alisema katika majeruhi hao, yupo mtoto aliyefahamika kwa jina la Ritwik Khaalelwal (13).
Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Vinod Suresh (37), Raj Rajin (30) na Prateek Javel ambaye umri wake haukufahamika mara moja.
Daktari huyo alisema majeruhi wengi wana vipande vya chuma mwilini na kwamba madaktari wanaendelea kuvitoa na hali zao zinaendelea vizuri.
MASHUHUDA WASIMULIA
Mashuhuda waliokuwa katika mgahawa huo wakipata chakula cha usiku, walisema ghafla walisikia kishindo kikubwa cha kitu kinachodaiwa ni bomu kikitokea dirishani na kutua chini ya meza moja walikokuwa wamekaa majeruhi hao na kulipuka na chembe chembe zake kusambaa katika mgahawa huo.
Walisema baada ya mlipuko huo, walipiga kelele kuomba msaada kwa kupigia marafiki simu ambao walifika kwa wakati na kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya Rufani ya Seliani.
Mmoja wa mashuhuda, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema muda mfupi baadae, polisi na vyombo vingine vya usalama vilifika eneo la tukio kufanyakazi ya uchunguzi wa awali.
Alisema saa 6.30 usiku, viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas walifika hospitali kuona hali za majeruhi hao.
Hilo ni tukio la sita kutokea jijini Arusha katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu na kusababisha vifo vya watu wanne na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
Mkazi wa Jiji la Arusha, Jabir Masoud aliulaumu uongozi wa mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mwenyekiti wake, Mulongo kwamba inastahili kubeba lawama kwa kushindwa kutoa majibu ya matukio hayo.
Alisema katika kila tukio, Kamanda  Sabas amekuwa akinukuliwa katika vyombo vya habari akisema  jeshi hilo limeingia kazini na muda mfupi watatoa taarifa ya uchunguzi, lakini hadi sasa hakuna kilichoelezwa wala kufanyika.
Masoud alisema Mulongo naye aliwahi kutamka katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Arusha (RCC), kilichofanyika Olasiti mwaka jana na kusema kuwa watataja majina ya wahusika hadharani, lakini hadi sasa hawajataja majina hayo.
KAULI YA DCI
DCI Mngulu alisema watu wawili wanahojiwa na polisi kufuatia tukio hilo na kwamba zaidi ya watu 25 wanatafutwa kutokana na kujihusisha na uhalifu wa kimataifa.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuusaka mtandao huo na vinajitahidi kuona nchi iko salama.
DCI Mngulu alisema matukio ya milipuko ya mabomu bado yanaendelea kujitokeza ambapo katika kipindi kifupi, mtu mmoja alifariki dunia mjini Zanzibar baada ya kulipukiwa na bomu kabla ya Shehe kulipukiwa na bomu.
“Pamoja na juhudi zinazofanyika, vitendo vya milipuko vinaendelea kutokea  kwenye baadhi ya maeneo yetu hapa nchini,” alisema.
Alisema katika tukio la juzi lililotokea Arusha, watu wanane wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na kwamba katika tukio la Zanzibar, watu 14 wanashikiliwa.
DCI Mngulu aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na kuwa macho na mikusanyiko isiyo ya lazima kutokana na walipuaji wengi kulenga kwenye maeneo yenye mikusanyiko.
Aliwataka wenye sehemu zinazokusanyika watu, wachukue tahadhari kwa kuweka vitu vya kisasa vya kukabiliana na milipuko.
AWAVAA CHADEMA
DCI Mngulu alisema viongozi wa CHADEMA hawana ushahidi wowote wa mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wao wa kampeni za udiwani jijini Arusha.
Alisema baada ya tukio hilo, viongozi wa CHADEMA walidai wana ushahidi na kutaka iundwe tume huru kuchunguza tukio hilo.
DCI Mngulu alisema tume zipo nyingi, ikiwemo ya Haki za Binadamu, wanaweza kutoa ushahidi wao na ukafanyiwa kazi.
“Wasisubiri mpaka iundwe tume fulani kwa ajili yao, zipo tume nyingi, wanaweza kwenda wakatoa ushahidi wao na ukafanyiwa kazi,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru