Tuesday 15 July 2014

Mtuhimiwa mtandao wa tindikali mbaroni


NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
JESHI la Polisi Zanzibar limemtia mbaroni mtuhumiwa wa mtandao wa tindikali, Alawi Mohammed Silima.
Ofisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohammed Mhina, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana na makachero wa polisi.
Alisema Silima (25), mkazi wa Fuoni Melinne nje kidogo ya mji wa Zanzibar, anahusishwa na tukio la kummwagia tindikali Sheha wa Shehia ya Tomondo, Mohammed Omar Said.
Mhina alisema mtuhumiwa huyo aliyekuwa akisakwa kwa muda mrefu, alikamatwa akiwa mafichoni eneo la Fuoni, baada ya taarifa za kiintelijensia kubaini kuwepo kwake.
Alisema makachero wa polisi wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ili kubaini mtandao mzima wa matukio mbalimbali yakiwemo ya tindikali yaliyotokea siku za hivi karibuni visiwani hapa. 
Kwa mujibu wa msemaji huyo, kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa za siri zilizotolewa na raia wema ambazo Jeshi la Polisi lilikua likiendelea kuzifanyia kazi chini kwa chini na kumbaini mtuhumiwa na mahali alikojificha.
Kutokana na kufanikiwa huko, alisema baadhi ya wananchi wa Zanzibar wamepongeza kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuliomba Jeshi la Polisi kuendelea na juhudi zake za kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika katika matukio mengine kama hayo visiwani hapa.
Mhina alisema sheha huyo, alimwagiwa tindikali Mei 22, mwaka jana,  alipokuwa akirudi nyumbani kwake akitoka kuchota maji katika nyumba ya jirani.
Alisema sheha huyo alijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mgongoni, kifuani, sikioni na jicho la upande wa kulia.
Hivi karibuni, watuhimiwa wengine 14 walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na mtandao wa kumwagia watu tindikali pamoja na ulipuaji wa mabomu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru