Wednesday 30 July 2014

Kumekucha Bunge la Katiba


NA MWANDISHI WETU
WAKATI  Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA), wakiendelea kukaidi matamko ya serikali na viongozi wa dini ya kuwataka kurejea bungeni, vikao vya bunge hilo litaanza rasmi Agosti 5, mwaka huu.


Wajumbe wanaounda kundi la UKAWA, ambao ni kutoka CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, walisusia vikao hivyo kwa madai ya kuwepo kwa upendeleo na ubaguzi.
Hata hivyo, baadaye walibadili hoja ya upendeleo na ubaguzi na kuibuka na mpya wakidai kuwa mgawanyo sawa wa wajumbe baina ya CCM ambayo ina wabunge wengi bungeni na vyama vya upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wote wametakiwa kuwasili mjini Dodoma kuanzia Jumapili ijayo.
Juzi, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wakati wa kuwasilisha salamu zake kwenye sherehe za Baraza la Idd El-Fitri lililofanyika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, limewataka wajumbe wa UKAWA kurudi bungeni kuendelea na mchakato.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye Baraza hilo lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, chama pamoja na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shabaan bin Simba.
BAKWATA imesema mamilioni ya shilingi za walipakodi zimetumika katika mchakato huo, hivyo kuuachia njiani ni usaliti na kitendo ambacho hakikubaliki.
Akiwasilisha salamu hizo mbele ya mamia ya mamia ya waumini wa dini ya kiislamu, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaj Suleiman Lolila, alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kususia bunge hilo ni pigo kwa Watanzania.
Alisema UKAWA wanapaswa kurejea bungeni kuendelea na majadiliano ili kuwawezesha Watanzania kupata Katiba Mpya na kuwa, iwapo kuna tofauti za mawazo au misimamo zinapaswa kujadiliwa ndani ya Bunge kwa kutumia Rasimu iliyowekwa mbele.
BAKWATA pia imeeleza kusikitishwa kwake kutokana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kushindwa kuyatilia maanani mapendekezo yake katika Rasimu Mpya ya Katiba.
Hata hivyo, imesema kuwa haitakata tamaa na badala yake itaendelea kuangalia namna bora ya kuwasilisha.
Kwa muda mrefu kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wajumbe wa Ukawa wanarejea bungeni baada ya kususia vikao. Viongizi wa serikali, taasisi za dini zote na asasi za kiraia, wanasiasa wamekuwa wakiwasihi wajumbe wa kundi hilo kurejea bungeni ili kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, kumewepo na tuhuma mbalimbali kuwa kundi hilo limekuwa likitumiwa na baadhi ya mataifa kwa lengo la kukwamisha mchakato huo.
Yapo madai pia baadhi ya wajumbe wamekuwa wakilipwa kati ya sh. 500,000 hadi milioni moja kwa siku kwa kususia vikao vya bunge hilo na kuendeleza vuguvugu la kuwarubuni wananchi ili wawaunge mkono.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru