Tuesday 15 July 2014

Bosi Bandari kortini



  •  Adaiwa kutoa zabuni kinyume cha sheria
  •  Ni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14 Dar  

NA FURAHA OMARY
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na Naibu wake, Hamad Koshuma, wamefikishwa  mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Vigogo hao wanadaiwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam  kwa China Communications Construction Company (CCCC), bila ya kutangaza zabuni.
Mgawe na mwenzake walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Washitakiwa hao walisomewa shitaka hilo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Isaya Arufani, na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti. 
Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya, akishirikiana na Wakili wa TAKUKURU, Benny Lincoln, na Wakili wa Serikali, Pius Hilla, ulidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, Desemba 5, 2011 katika Mamlaka ya Bandari Tanzania, Dar es Salaam.
Lincoln alidai washitakiwa wakiwa waajiriwa na mamlaka hiyo, wakiwa na nafasi ya mkurugenzi mkuu na naibu mkurugenzi mkuu katika utekelezaji wa majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutia saini mkataba wa biashara kati ya TPA na kampuni hiyo ya China.
Alidai mkataba huo ulikuwa wa upanuzi wa magati namba 13 na 14 katika bandari hiyo, bila kutangaza zabuni jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma. Lincoln  alidai kitendo hicho kililenga kuipatia faida kampuni hiyo ya China.
Washitakiwa  hao wanaotetewa na Wakili Samson Mbamba, walikana shitaka ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mbamba aliomba dhamana kwa washitakiwa kwa kuwa shitaka linalowakabili linadhaminika kisheria. Ombi hilo halikupingwa na upande wa Jamhuri, hivyo Hakimu Arufani alitoa masharti ya dhamana.
Masharti hayo ni kila mshitakiwa kutia saini bondi ya sh. milioni mbili na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaotia saini bondi hiyo.
Washitakiwa hao walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Agosti 13, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Upanuzi huo wa gati namba 13 na 14, ulizua mzozo na kusababisha  aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu na Naibu wake, Athuman Mfutakamba kuondolewa katika nyadhifa zao na nafasi hizo kuchukuliwa na Dk. Harrison Mwakyembe na Dk. Charles Tizeba . 
Viongozi hao walionmdolewa mwaka juzi wakati Rais Jakaya Kikwete alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Katika sakata hilo, Nundu alimtuhumu  Mfutakamba kwamba alikuwa akishinikiza  CCCC ipewe kazi ya kujenga magati hayo, kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje ya nchi.
Baada ya kuingia katika nafasi hiyo Dk. Mwakyembe alifanya mabadiliko yakiwemo ya kuwasimamisha kazi maofisa kadhaa wa TPA.
Miongoni mwa waliotangazwa kusimamishwa kazi walikuwa Mgawe na manaibu wake wawili ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zinawakabili zikiwemo za kupotea kwa mafuta na kuidanganya serikali kuhusu mafuta machafu na masafi. 
Dk. Mwakyembe aliunda tume ya watu saba kufanya uchunguzi kwa wiki mbili na kupeleka taarifa ofisini kwake
Taarifa hiyo ya uchunguzi ilimwezesha Dk. Mwakyembe, Januari 21, 2013, kutangaza kuwatimua kazi vigogo watano wa TPA, wakiwemo Mgawe na Koshuma.
Akitangaza uamuzi huo, Dk. Mwakyembe alitaja mbele ya waandishi wa habari tuhuma za kila mmoja aliyetimuliwa, ambapo Mgawe na Koshuma, miongoni mwa tuhuma zao ilikuwa kukiuka sheria na utaratibu kuhusiana na upanuzi huo.
Dk. Mwakyembe alisema Mgawe na Koshuma waliingia mkataba na kampuni hiyo bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.
Hata hivyo, Desemba 28, 2012,  CCCC ilifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Biashara dhidi ya TPA, Waziri wa Uchukuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuomba kuizuia serikali kuchukua hatua yoyote ya kutangaza zabuni ya upanuzi wa bandari.
Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Agnes Bukuku, ambapo  CCCC iliiomba mahakama kuzuia serikali kutangaza zabuni hiyo  hadi mgogoro uliokuwepo katika Baraza la Usuluhishi la Ujenzi utakapomalizika.
Kwa mujibu wa hati yao ya madai, CCCC walidai katika mkataba walikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro, watakwenda Baraza la Usuluhishi la Ujenzi kusuluhisha.
Inadaiwa serikali ilitoa zabuni ya upanuzi wa bandari kwa kampuni ya CCCC, lakini kabla haijaanza kufanya kazi, ilibainika kuwa kampuni hiyo ilikuwa na matatizo na ikafungiwa China. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru