Wednesday 30 July 2014

Tibaijuka: Nimejipanga kutimiza ahadi zangu


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka, amesema mikakati aliyojiwekea kwa sasa ni kutimiza ahadi alizowapa wapigakura na kutekeleza Ilani ya Uchanguzi ya CCM ya mwaka 2010.
Aliyasema hayo kwenye ziara ya Rais Jakaya Kikwete mikoa ya kusini mwa Tanzania, ambako walipokewa kwa shangwe na kundi la wananchi kutokana na kufanikiwa kutatua kero nyingi za ardhi zilizokuwa katika maeneo yao.
Utatuzi huo ulihusisha pia kumnyang’anya ardhi mwekezaji ambaye alikuwa akitaka kuendelea kuhodhi eneo kubwa  lililopaswa kumilikiwa na wananchi.
Sambamba na hilo, Profesa Tibaijuka alipongezwa na wananchi hao wa mikoa ya Lindi na Ruvuma kwa kulisimamia kwa makini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika utekelezaji wa majukumu hali iliyosaidia kuongeza ufanisi katika uanzishaji wa miradi katika mikoa mbalimbali nchini.

“Kwa kazi inayofanywa na NHC, kweli Waziri Tibaijuka amefanya kazi. Miradi inayoendelea kutekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kote nchini, ni chachu ya maendeleo na bila shaka miji yote itakuwa imepangika kama tulivyowahi kuota baadhi ya Watanzania juu ya mipango miji inayoeleweka katika nchi yetu,” alisema mmoja wa wananchi hao.   
Hata hivyo katika ziara hiyo, Rais Kikwete alisema serikali inamjali kila Mtanzania bila kujali eneo alipo tofauti na ilivyoaminika miaka kadhaa iliyopita, kuwa haitoi kipaumbele kwenye mikoa ya kusini.
Mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alizindua ghala la mahindi ambalo litahifadhi tani 5,000 za mahindi ya ukanda huo, ambayo awali yalikosa hifadhi kutokana na kuongezeka kwa mavuno msimu huu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru