Saturday, 12 July 2014

SMZ kuimarisha ufugaji wa samaki


NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema azma yake ya kuimarisha ufugaji wa samaki nchini inatekelezwa kikamilifu na itaendelea kutoa mafunzo na huduma kwa wananchi ili wajiimarishe kiuchumi na kuchangia pato la taifa.
Rais wa Zanzibar, Dk, Ali Mohamed Sheni, alisema hayo juzi alipozungumza na vikundi vya ushirika wa ufugaji samaki vya Hakiliki katika eneo la Mwambe, Wilaya ya Mkoani na Siri Salt and Fish Farm cha Pujini, wilayani Chakechake.
Alisema serikali inaipa uzito mkubwa sekta ya uvuvi ikiwemo shughuli za ufugaji wa samaki unaofanywa na wananchi.
Dk. Sheni alibainisha kuwa, jitihada zimekuwa zikifanyika kuendeleza shughuli za ufugaji wa samaki Unguja na Pemba na kwamba, kwa kushirikiana na serikali za China na Korea Kusini, itaanzisha vituo vya utafiti ambavyo vitajumuisha utotoaji wa vifaranga vya samaki.
Aliwaeleza wanachama wa vikundi hivyo na wananchi waliokuwepo alipotembelea vikundi hivyo kuwa kituo kimoja kitajengwa Mkokotoni Unguja na kingine Pemba katika Kijiji cha Ukunjwi.
Sheni alisema lengo la serikali ni kuhakikisha changamoto zinazoikabili sekta hiyo zinapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Dk. Kassim Gharib, alisema kuanzishwa kwa vituo vya utafiti  kutasaidia kufanyika utafiti kuhusu aina nyingi zaidi za samaki wanaoweza kufugwa tofauti na sasa ambapo wanaofugwa ni perege na mwatiko.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru