Monday, 21 July 2014

SUMATRA yalia na wanasiasa


NA MOHAMMED ISSA
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imesema tatizo la usafiri wa pikipiki nchini linachangiwa na utashi wa kisiasa.
Pia imesema ajali za pikipiki zimekuwa tishio na kwamba zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.
Mbali na hilo, imesema asilimia 99 ya watoa huduma ya usafiri wa pikipiki, hawana leseni na kwamba, hawana elimu ya usafiri.
Imesema kutokana na hali hiyo, hivi karibuni itaanza kutoa elimu nchi mzima na haitatoa leseni ya usafiri wa pikipiki kwa mtu ambaye hajapata elimu na kukidhi vigezo.
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliad Ngewe, alisema hayo jana ofisini kwake mjini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.
Profesa Mwandosya jana aliitembelea mamlaka hiyo na kupata maelezo ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUMATRA.
Ngewe alisema utashi wa kisiasa ni moja ya changamoto inayowakabili katika usafiri wa pikipiki na kwamba wanatarajia kutoa elimu kwa wanasiasa ili waweze kufahamu taratibu za kiusafiri.
Alisema elimu hiyo inatarajiwa kutolewa kwa wananchi kwenye maeneo yote nchini  ili kila mtoa huduma ya usafiri wa pikipiki, aweze kupata  elimu kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo.
Ngewe alisema mamlaka hiyo imeanza kujipanga kuhakikisha inalipatia dawa tatizo la ajali, zikiwemo za pikipiki ambazo zinazidi kuongezeka siku hadi siku.
Alisema elimu hiyo itasaidia madereva wa pikipiki kuona umuhimu wa kuwa na leseni pamoja na wajibu wa abiria anapopakiwa kwenye usafiri huo.
Ngewe alisema utafiti unaonyesha ajali nyingi za pikipiki zinatokana na madereva wa vyombo hivyo kukosa elimu.
Alisema kuanzia sasa waendesha pikipiki wanalazimika kapata mafunzo mpaka watakapokidhi viwango ndio waanze kupewa leseni za kutoa huduma.
MWANDOSYA: ACHENI WOGA
Waziri huyo aliwaagiza viongozi na watendaji wa SUMATRA, kuacha uoga katika kusimamia majukumu yao kwa kuhofia wanasiasa.
Alisema ni lazima wahakikishe uhai wa watu kuliko kufikiria ajira za watu kama wanavyotaka baadhi ya wanasiasa.
“Wanasiasa wao kila siku wanasimamia ajira zao, lakini nawaomba nyinyi msimamie maisha ya watu kwanza bila ya uoga wowote,” alisema.
Akizungumzia usajili wa meli unaofanywa Zanzibar na Tanzania Bara, Profesa Mwandosya alisema hakuna mgogoro wowote na suala hilo linazungumzika.
Alisema suala la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kutoa vibali vya usajili wa meli ni la ndani na linataka ushirikiano wa pande zote mbili.
Alisema wakati umefika sasa kuwe na utaratibu kwamba upande mmoja ukitoa kibali cha kusajili meli, mwingine uwe na taarifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru