Tuesday, 15 July 2014

Mgogoro wafukuta Moravian  • Wachungaji, waumini wafunga ofisi ya Askofu
  • Kazi zasimama kwa saa nne, Polisi waingilia kati

NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MGOGORO unaoendelea kufukuta ndani ya Kanisa la Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, umechukua sura mpya baada ya wachungaji na waumini kufunga ofisi ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Alinikisa Cheyo, kwa makufuli na minyororo.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni shinikizo la kumtaka Askofu Cheyo, ajiuzulu wadhifa huo kutokana na madai ya kumfukuza kazi Mwenyekiti wa jimbo hilo, Mchungaji Nosigwe Buya, bila kufuata taratibu za kanisa.
Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kushangaa, lilitokea jana saa 12;00 asubuhi katika ofisi za kiongozi huyo wa juu wa kanisa zilizoko Jacaranda, jijini Mbeya.
Sakata hilo la aina yake, lililoibua maswali mazito juu ya mustakabali wa kanisa hilo, lilisababisha shughuli zote katika eneo hilo kusitishwa huku baadhi ya wafanyakazi wakilazimika kukaa nje ya lango kuu kwa kukumbwa na sintofahamu. 
Polisi walilazimika kufika eneo la tukio na kuimarisha ulinzi hadi saa 3:15 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla, alipofika na kuwaomba waumini kutuliza jazba na kufungua minyororo pamoja na makufuli waliyokuwa wameyafunga.
Dk. Sigalla aliwataka waumni hao wapunguze jazba na kuwa serikali  inalitambua tatizo hilo hilo na kuahidi kesho (leo), kuitisha kikao cha Kamati ya Halmashauri Kuu ya Kanisa, Askofu, Mwenyekiti na Wachungaji ili kujua hatima ya kuitishwa kwa mkutano mkuu wa kanisa na kufanya uamuzi sahihi.
Mchungaji wa Kanisa la Moravian, Ushirika wa Bethelehem, Joseph Mwakyoma, alisema wamelazimika kuchukua uamuzi huo, kutokana na kuchoshwa na vitendo anavyovifanya Askofu Cheyo kwa kujichukulia uamuzi mzito wa kumsimamisha Mwenyekiti Mchungaji Buya kwa tuhuma za kufuja sh. milioni 600 za kanisa.
Mchungaji Mwakyoma aliongeza kuwa kulingana na tuhuma hizo, kanisa liliunda tume ili kubaini ukweli ambapo ilionekana Mwenyekiti Buya, hahusiki na ubadhirifu wa fedha hizo.
“Tuliomba kanisa liitishe mkutano mkuu (Sinodi), ili waumini waweze kujua hatima ya mwenyekiti  wao, ambaye hadi sasa amesimamishwa kazi kwa kipindi cha mwaka sasa, na kumtaka Askofu Cheyo ajiuzulu wadhifa wake,” alisema Mchungaji Mwakyoma.
Kwa mujibu wa Mchungaji Mwakyoma, wanashindwa kuelewa nini hatima ya mwenyekiti wao kwa kuwa kila wanapoomba mkutano mkuu uitishwe, Askofu Cheyo amekuwa haafiki na kuongeza serikali iliingilia kati na kuagiza mkutano mkuu uitishwe, lakini mpaka hadi sasa hakuna kinachoendelea.
Aliongeza kuwa kwa nafasi yake, Askofu Cheyo ni kama mshauri na kiongozi wa kanisa hivyo hapaswi kuingilia shughuli za kiutendaji za kanisa na kwamba kwa hali mgogoro huo kuzidi kukomaa, kuna uwezekano mkubwa wa damu kumwagika. 
Kwa upande wake, mmoja wa Wazee wa Kanisa aliyejitambulisha kwa jina la Israel Jengela, alisema  malumbano yaliyoibuka katika kanisa hilo yanapaswa kumalizwa  kwa kiongozi huyo wa kanisa kuitisha mkutano mkuu ili kuondoa tofauti zilizopo kati yake na mwenyekiti ili kanisa liweze kuongozwa kwa maadili ya kiroho  na si kugawa waumini katika makundi. 
Awali, Mchungaji Mwampanga alipohojiwa kuhusiana na uamuzi wa  waumini na wachungaji kufunga ofisi za kanisa hilo, alisema wanaofanya hivyo ni waumini wachache na kwamba Askofu Cheyo hana matatizo yoyote bali mwenyekiti amekuwa akikumbatia watu wanaofuja fedha za kanisa.
Mwampanga alidai anachotambua ni kuwa Askofu hana makosa yoyote, bali Halmashauri Kuu ya Kanisa ilibaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha na kuwa Mchgungaji Buya, alipotakiwa kuwaita wahusika alikuwa anapiga chenga, hali iliyosababisha kusimamishwa kazi. 

Juhudi za kumpata Askofu Cheyo ili aweze kulitolea ufafanuzi suala hilo hazikuweza kuzaa matunda kwani simu yake ya mkononi ilipopigwa ilikuwa inaita tu bila majibu. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru